CURRENT NEWS

Friday, November 4, 2016

RC NDIKILO:WALIOVAMIA HIFADHI YA UZIGUA WAONDOKE MARA MOJA/AGIZO HILO LAMSABABISHIA MSAFARA WAKE KUWEKEWA MAGOGO BARABARANI


Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza jambo wakati ilipokwenda kutembelea hifadhi ya msitu wa Uzigua na kutoa agizo kwa waliwavamia waondoke Mara moja(Picha  zote  na Mwamvua Mwinyi)


Magogo yaliowekwa kuzuia  msafara wa mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo yakionekana kuwekwa kando ya njia itokayo Kwakonje kuelekea kwenye hifadhi ya msitu wa Uzigua,wavamizi katika msitu huo walisema magogo hayo baada ya mkuu huyo kutoa agizo la  kuwataka  waondoke (picha na Mwamvua Mwinyi)

4,nov
Na Mwamvua Mwinyi,Kibindu

MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo,amewataka watu waliovamia hifadhi ya msitu wa Uzigua upande wa wilaya ya Bagamoyo kuondoka mara moja katika hifadhi hiyo na atakaekaidi ataondolewa kinguvu.

Kufuatia kutoa agizo hilo baadhi ya watu hao waliamua kuuzuia msafara wake kwa kuweka magogo katikati ya njia itokayo kijiji cha Kwakonje ,kata ya  Kibindu kuelekea kwenye hifadhi ya msitu huo .

Aidha amemuasa mwenyekiti wa kijiji cha Kwakonje ,Omary Haji Mbwana,kuacha tabia ya kushawishi wavamizi hao kuwa wagomee kuhama kwenye hifadhi hiyo na afuate miongozo na miiko ya kazi zake ili kuondoa migongano baina ya serikali na wananchi.

Akiwa ameambatana na ujumbe kutoka ofisi ya serikali ya mkoa,wilaya na wakala wa misitu (TFS)kanda ya Mashariki na Bagamoyo,walipatwa na mkasa huo baada ya kwenda kujionea uharibifu wa mazingira uliopo hali iliyosababisha uoto wa asili na vyanzo vya maji kuondoka.

Mhandisi Ndikilo,alisema watu hao waliingia kwenye msitu huo bila utaratibu na kinyume cha sheria hivyo wanapaswa kuondoka na kwenda kutafuta maeneo mengine.

“Msitu huu wa Uzigua hatakiwi kukaa mtu wala kulima,kukata miti ovyo,nawaomba muondoke bila shuruti ili kurejesha uoto wake wa asili ambao uwetoweka pamoja na mto wa WAMI uweze kupata maji”

"Anzeni kufunga virago muanze safari ya kurudi huko mlikotoka,saa ndio imefika hakuna ajizi"alisema mhandisi Ndikilo.

Hata hivyo alielezea kuwa wavamizi wote kutoka upande wa wilaya tatu zinazozunguka msitu huo,Kilindi,Handeni na Bagamoyo walishapewa tangazo la kuhama tangu mwaka 2014 .

Alisema hadi sasa wavamizi upande wa Kilindi na Handeni wameshaondoka ambao waliobakia ni wilaya ya Bagamoyo .

Alieleza kutokana na maagizo na elimu ya mara kwa mara ilishawahi kutolewa kupitia wakala wa misitu na wilaya ya Bagamoyo hivyo hawezi kuongeza muda  kinachotakiwa ni kila alievamia kuanza kutii mamlaka pasipo kushurutishwa.

Mhandisi ndikilo aliiasa jamii hiyo kuacha kupimana ubavu na serikali na kuwaomba watekeleze maagizo ya serikali na sio vinginevyo.

Kuhusiana na watu wanaodai kuwa waliuziwa maeneo ya msitu na kijiji anasema suala hilo lipo nje ya mipango ya serikali aliyeuziwa ametapeliwa na imekula kwake.

Akizungumzia kitendo cha kuwekewa magogo kwenye msafara wake ,aliwataka wananchi hao kuacha mambo ya uhuni na mzaha kwa serikali inapoamua kutekeleza majukumu yake .

Alimuagiza mkuu wa kituo cha polisi Chalinze kumfungulia jarada mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Amos anaedaiwa kushawishi wenzie kuweka magogo katika msafara huo.


Mhandisi Ndikilo,alikemea tabia ya mwenyekiti wa kijiji cha Kibindu kushawishi wananchi wakaidi maagizo ya serikali ambapo taratibu za kiuwajibishaji zitafuata ili iwe fundisho kwa viongozi wengine.

Nae mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ,alhaj Majid Mwanga,alisema wameshawahi kwenda kuzungumza na wananchi hao na walitakiwa waondoke tangu mwezi april mwaka huu ambapo waliongezewa muda hadi mwezi sept/oct.

Alisema muda walioongezewa umeisha lakini bado wanaonekana kutoa vikwazo na kuomba kuongezewa muda.

Alhaj Mwanga alielezea kwamba ifikie hatua jamii ikawa na uelewa wa makusudio ya serikali yao na kuachana na tabia ya kutaka kuhalalisha mambo yasiyokuwepo.

Alisema kila mmoja anajua kama alivamia na ni eneo la msitu lakini wanachotaka kufanya kwasasa ni kushindana na serikali na kutaka kuhalalisha uwepo wao kwenye hifadhi.

Kwa upande wake ,afisa msaidizi wa misitu Bagamoyo,Jonathan Mpangala,alisema msitu huo ulitangazwa na serikali kwa tangazo namba 466 ,la mwaka 1958.

Alisema kuna wilaya tatu zilizoingilia msitu huo ikiwemo vijiji nane vya wilaya ya Bagamoyo,vijiji viwili wilaya ya Kilindi na Handeni ni kijiji kimoja .

Mpangala alisema wakala wa misitu ulipoanza mwaka 2014 ndipo msitu wa Uzigua ulipimwa tena rasmi ,ukiwa na ukubwa wa hekta 24,436 ama kwa tafsiri ya hekari 61,090 ambako katika kipindi hicho walitoa tangazo la kuwataka wavamizi waondoke.

Alieleza  kuna kaya 3,000 hadi sasa zinazoishi kwenye msitu huo nje ya utaratibu,vibanda vya nyasi wanazoishi watu hao na mifugo mbalimbali 6,000.

Baadhi ya watu hao ,waliomba serikali iwasaidie kuwapa eneo jingine la kuishi kutokana na kwamba wengi wao wametoka Kazimzumbwi na mikoa mbalimbali ambayo ipo mbali kama Kigoma,Kagera,Singida na Mwanza.
 
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania