CURRENT NEWS

Wednesday, November 23, 2016

SERIKALI YAWAONYA WAAJIRI WASIOTOA MIKATABA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua mkutano mkuu wa sita wa Shrikisho la Vyama vya wafanyakazi nchini(TUCTA), uliofanyika leo mjini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki akizungumza katika Mkutano mkuu wa Tucta uliofanyika mjini Dodoma.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi Ajira na Vijana na watu wenye ulemavu  Jenista Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana na viongozi wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA), wakishiriki kuimba wimbo wa wafanyakazi kwenye Mkutano mkuu wa Tucta uliofanyika mjini Dodoma.


Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini(TUCTA), Gratian Mkoba akizungumza katika mkutano mkuu wa shirikisho hilo uliofanyika mjini Dodoma.

.................................................................................................
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haitawavumilia waajiri ambao hawatoi mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao na amewaonya waache tabia hiyo mara moja.

Ametoa agizo hilo leo  wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) katika ukumbi wa Mwalimu Julius K. Nyerere ulioko Chuo cha Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

 “Nitoe wito kwa waajiri wote ambao wamekuwa na tabia ya kutokutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao, waache tabia hiyo mara moja, kwani Serikali haitamvumilia mwajiri wa namna hii,” ameonya.

Akijibu hoja ya waajiri kutokutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi ambayo iliibuliwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu amesema kifungu cha 14 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004  kinaelekeza aina mbalimbali za mikataba inayotakiwa kutumika kuajiri wafanyakazi. 

“Kisheria mwajiri anao wajibu wa kuhakikisha kila mtumishi wake ana mkataba wa kazi kwa maandishi,” amesisitiza.
Ameongeza “Pia ninawaagiza maafisa wa kazi wanaohusika na kaguzi za kazi kote nchini, wahakikishe kila mwajiri anafikiwa wakati wa ukaguzi na hatua stahiki zinachukuliwa kwa wote wasiotekeleza matakwa ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.


Amesema haki ya mfanyakazi na ndiyo ufunguo wa mahusiano mema yanayoweza kuleta utulivu, amani, kuongeza tija na uzalishaji sehemu ya kazi.

Akijibu hoja kuhusu wafanyakazi kuwekwa ndani kiholela, kunyanyaswa, kushushwa vyeo na kusimamishwa kazi na wanasiasa, Waziri Mkuu amesema Serikali chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora ili kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi zinalindwa ipasavyo.

”Kimsingi watumishi wanasimamiwa na mamlaka za kinidhamu na sheria mbalimbali ambazo hazina budi kuangaliwa kwa pamoja kabla ya kuchukua hatua. Ninawaagiza viongozi wenzagu wa kisiasa na walioko katika wizara na taasisi zote za Serikali, mikoani, wilayani, kwenye idara za Serikali na Halmashauri wazingatie utawala wa sheria wakati wa kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi,” amesema huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo

Mbali na hilo, risala ya shirikisho hilo iligusa maeneo mengine kama vile watumishi wa umma kutopandishwa vyeo kwa wakati muafaka; walitaka kujua bodi za mishahara za kisekta zitaanza kazi lini; kukosekana kanuni za uandikishwaji wa vyama vya wafanyakazi na waajiri; marekebisho ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na ucheleweshwaji wa malipo ya pensheni; haja ya kuoanisha Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.

Akijibu baadhi ya hoja hizo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi Ajira na Vijana na watu wenye ulemavu  Jenista Mhagama amesema dhana ya utatu baina ya wafanyakazi, waajiri na Serikali ndiyo nguzo kuu ya kukuza uchumi wa Tanzania.

Akifafanua kuhusu fao la kujitoa, Waziri Mhagama alisema baada ya uongozi wa TUCTA kukamilika, itabidi wakutane na kukaa pamoja kuainisha sera inataka nini na hali ya uchumi ya sasa ikoje huku wakiangalia dhana nzima ya hifadhi ya jamii nayo inataka nini.

“Kuna haja ya kuangalia sera inataka nini, tunapaswa tuangalie mabadiliko ya kiuchumi katika nchi yetu na kutazama dhana nzima ya hifadhi ya jamii kwenye maisha yetu ya uzeeni. Tukikaa pamoja, yaani, mwajiri, mfanyakazi na Serikali, tutapata njia ya kisheria ya kuweza kulifunga jambo hili ili lisiendelee kuwa kero kwa wafanyakazi wetu,” amesema.

Akijibu hoja kuhusu suala la watumishi kutopandishwa vyeo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki amesema kwa kipindi cha miaka mitano jumla ya watumishi 343,689 walipandishwa vyeo ikiwa ni kuanzia mwaka 2011 hadi 2016. Hata hivyo, alisema wanakabiliwa na changamoto ya watumishi wengine kutokidhi vigezo.

“Kuna baadhi ya watumishi hawakidhi vigezo vya maendeleo na masharti vya muundo wa masharti ya utumishi wa umma. Tumetoa maelekezo kuwa wale waliokosa vigezo na wamekaa muda mrefu bila kupandishwa vyeo, wapewe mafunzo na bajeti zitengwe ili waweze kutimiza vigezo vya muundo wa utumishi wa umma,” amesema.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Kenya (COTU), Bw. Francis Atwoli amesema anaikubalia kasi ya Rais Magufuli katika kupambana na rushwa na kuwataka Watanzania wamuunge mkono badala ya kulalamikia kasi kwani wao wanatamani mwakani aende kugombea kwao katika uchaguzi mkuu ujao.

“Ninawasihi wanaTUCTA suala la rushwa msilipe nafasi. Mpambane nayo kwa sababu kule kwetu imeota mizizi. Muungeni mkono Rais Magufuli, badala ya kulalamika kuwa kasi yake ni kubwa mno. Mnasema eti ana spidi sana, mkiona taabu mtuazime japo kwa mwaka mmoja ili aje atunyooshee mambo kule kwetu,” amesema huku akishangiliwa.

Amewataka wahimize uhusiano uliopo baina ya vyama vya wafanyakazi, waajiri na Serikali iliyopo madarakani na kuwataka wadumishe umoja miongoni mwa viongozi na wanachama mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi.

“Msiruhusu mgawanyiko wa makundi baada ya uchaguzi sababu hauwasadii wafanyakazi ambao ni wanachama wenu. Mmeona madhara ya kuendeleza makundi kule nchini kwetu, msiruhusu hayo yatokee hapa,” ameonya.

TUCTA inatarajiwa kufanya uchaguzi wake  Novemba 24, 2016 na kuchagua uongozi mwingine utakaongoza kwa kipindi cha miaka mitano. 


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania