CURRENT NEWS

Thursday, November 24, 2016

WAVAMIZI TAALUMA YA ‘FIZIOTHERAPIA’ KUSHTAKIWA


Na Mwandishi Wetu
Serikali imesema itachukua hatua kali ikiwemo kuanza kuwashtaki wavamizi wote wa taaluma ya tiba ya viungo vya mwili ijulikanayo kama ‘fiziotherapia’ baada ya kubaini uwepo wa wimbi kubwa la watu wasio na sifa ya kuhudumu tasnia hiyo
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Bakari Kambi, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa wanachama wa Fiziotherapi nchini (APTA) Dar es Salaam.
Alisema serikali kupitia wizara ya Afya ipo mbioni kukamilisha mchakato wa kutunga sheria mpya itakayohusika kudhibiti wavamizi na wachafuzi wa tiba hiyo muhimu ambao wametapakaa maeneo mbalimbali nchini baada ya ile ya awali kuonyesha baadhi ya mapungufu.
“Muswada wa sheria mpya ambayo tuko mbioni kuikamilisha itatambua rasmi taaluma hii muhimu na nyinginezo kama taaluma ya meno, na sayansi za afya shirikishi chini ya bodi itakayoundwa ili kudhibiti mwenendo wake hatua kwa hatua,” alisema Profesa Kambi.
Aidha, aliwataka mafiziotherapia waliopo nchini kote wapatao 350 kuonyesha mshikamano wao kwa kujiunga pamoja ndani ya APTA ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowahusu, kukabiliana na mianya ya uchafuzi wa taaluma hiyo na kuiwezesha serikali kuwafikia kwa urahisi.
Pamoja na mambo mengine, Mganga Mkuu aliwakumbusha kufanya kazi yao kwa kuzingatia maadili, huku akisisitiza kuwa kinyume chake wataripotiwa kwa njia yoyote ile..kwani dunia ya leo haina siri na inakwenda kiteknolojia zaidi hasa kwenye eneo la upashanaji habari.
“Msikubali mmoja wenu awachafue toeni taarifa tuchukue hatua mara moja, fanyeni kazi zenu kwa weledi kumbukeni mpo kwenye nchi inayokua kwa kasi kiteknolojia mkiharibu mtakutana na wanasheria wengi mitaani wanaotafuta kesi, na bado mtarekodiwa na taarifa zenu kusambazwa mitandaoni,” alisema.
Kwa upande wake, Rais wa APTA, Remla Shirima, alisema taaluma hiyo iliyoanzishwa tangu mwaka 1948 hadi sasa ina wafiziotherapia 350 tu waliosajiliwa huku ikikabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo wataalamu na vifaa tiba.
Mwisho


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania