CURRENT NEWS

Tuesday, November 22, 2016

WAWILI WAUAWA RUFIJI HUKU MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI IKIHUSISHWAWATU wawili wakazi wa Kilimani kata ya Ngorongo tarafa ya Mkongo wilayani Rufiji mkoani Pwani, wameuawa kwa nyakati tofauti ,mauaji ambayo yanahusishwa na migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Katika mauaji hayo mfugaji aliuawa kwa kupigwa mawe kisha kuchomwa moto na mkulima kuuawa na kutupwa kandokando ya mto.
Aidha jeshi  la  polisi mkoani Pwani linawatafuta watu watatu kutokana na mauaji hayo na walikimbia baada ya kutenda kosa  hilo.
Akizungumzia kuhusiana na matukio hayo ,kamanda wa polisi mkoani Pwani ,Boniventure Mushongi ,alisema tukio la  kwanza, Muhidini Said Mpange (23)mkulima na mkazi wa Kilimani alikutwa ameuawa pembeni mwa  mto  Rufiji kwenye shamba la  mahindi la  Ally Ngahama.
Alieleza kuwa  tukio hilo lilitokea ,juzi majira ya saa mbili asubuhi huko maeneo ya Nyasule ,kijiji cha Kilimani Magharibi kata ya Ngorongo wilayani humo.
Kamanda Mushongi alisema mwili wa marehemu umekutwa ukiwa na majeraha katika maeneo mbalimbali  ya mwili wake.
Alisema kwamba uchunguzi wa awali umebaini mauaji hayo yametokana na marehemu kudai fidia ya uharibu wa mazao yake baada ya mifugo kuingia.
Kamanda huyo alifafanua kuwa katika tukio jingine,mnamo novemba 20 majira ya saa  4 asubuhi huko Kilimani,mfugaji aitwae Jugi Makono Bushini (25)mkazi wa Ngorongo aliuawa kwa kupigwa na mawe sehemu mbalimbali  za mwili kisha kuchomwa moto.
"Uchunguzi wa awali tumeweza kubaini kuwa tukio hilo lilikuwa na lengo la  kulipiza kisasi kutokana na mauaji ya mkulima yaliyofanywa na wafugaji .
Hata  hivyo kamanda Mushongi alisema kutokana na matukio hayo tayari timu  ya makachero wa mkoa ipo  huko ikiongozwa na mkuu wa upelelezi SSP Mbise kwa lengo la  kutafuta kiini cha mgogoro huo .
Alisema pia wanatafuta ufumbuzi ikiwepo  na kuwasaka wale wote  waliohusika kwenye vifo  hivyo na kuweza kuwachukulia hatua za kisheria.
Alitoa rai kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi na pale panapojitokeza matukio ya ukiukwaji wa sheria kwenye maeneo yao watatumie mabaraza ya vijiji ama kata katika kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania