CURRENT NEWS

Friday, November 25, 2016

WAZIRI MWAKYEMBE:KUWALIPIA WAFUNGWA FAINI KUNA HATARI YA KUPOTOSHA MFUMO WA ULIOPO WA HAKI JINAI

Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe

Serikali imesema utaratibu ulioanza kujitokeza nchini wa baadhi ya asasi za kidini na wananchi kuyalipia faini makundi ya wafungwa magerezani, una hatari ya kupotosha dhamira na dhana nzima ya adhabu katika mfumo uliopo wa Haki jinai.
Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amesema hayo jijini Dar es Salaam na kusema  dhana na dhamira ya adhabu kwa makosa ya jinai ni kumfanya aliyetenda kosa ajutie kosa lake na wengine wenye mwelekeo kama wa kwake katika jamii, wajifunze na wajirekebishe ili nao yasije yakawakuta.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari ofisini kwake  kuhusu malalamiko ya Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Agustino Mrema kuwa waliolipiwa faini bado mpaka leo hawajaachiwa, Waziri huyo alimpongeza Kamishna Mkuu wa Magereza, John Minja, kwa kutotetereka katika kusimamia sheria.
Amesema kulipiwa faini kwa makundi na watu wasio na nasaba moja kwa moja na wafungwa, kunaondoa  kabisa lengo la adhabu la kumfanya mkosaji ajutie kosa lake na wengine katika jamii waliokuwa na mwelekeo huo kujirudi.
Ameongeza kuwa pamoja na nia njema ambayo walipa faini hao wanaweza kuwa nayo, usamaria wema huo umweza kuchochea uvunjaji zaidi wa sheria kwa imani kuwa kuna mtu baadaye atakaye watoa kwa pesa bila wao au ndugu zao wa karibu kutoa jasho lolote.
Hivi karibuni Kanisa la Assemblies of God (Mlima wa Moto) Mikocheni B Dar es Salaam liliwalipia faini wafungwa kadhaa katika magereza ya Keko, Segerea na Ukonga Dar es Salaam na gereza la Isanga, Dodoma.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Parole, Mhe. Augustine Mrema, amesikika akiulaumu uongozi wa Magereza nchini kwa kuendelea kuwashikilia wafungwa waliolipiwa faini na hivyo kuongeza msongamano magerezani.

Idara ya Magereza nayo inajitetea kuwa kuwa hata baada ya kulipiwa faini, lazima ijiridhishe na matakwa ya sheria ya haki jinai.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania