CURRENT NEWS

Tuesday, November 15, 2016

WAZIRI UMMY-WALIOANZISHA VYUO VYA UUGUZI KAMA VITEGA UCHUMI KUFUTWA

Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha 
WAZIRI wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto ,Ummy Mwalimu amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaoanzisha vyuo hewa vya uuguzi kama vitega uchumi badala ya kufuata vigezo stahiki katika utoaji elimu wa fani hiyo.
Aidha amesema vipo baadhi ya vyuo hivyo ambavyo havijasajiliwa na wanafunzi wanalipa ada ambapo wakati wa  mitihani ya mwisho ya wanachuo wanashindwa kuifanya hivyo kuwa sawa na kutapeliwa.
Kutokana na kuibuka kwa vyuo hewa ya uuguzi ,Ummy ametoa agizo la kuvifuta vile ambavyo vinaonekana kwenda kinyume na taratibu zilizopo. 
Aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la kituo cha kuendeleza wauguzi na wakunga nchini . 
Ummy alisema kumekuwa na idadi kubwa ya vyuo feki ambavyo vimefanywa kama sehemu ya ujasiriamali kwa wanaovianzisha kujipatia fedha. 

Alieleza kuwa kuna kila sababu ya kufanya maamuzi yenye tija ili kupunguza idadi kubwa ya vyuo vya uuguzi ambavyo husababisha malalamiko kutoka kwa wagonjwa kutokana na wahitimu kutokidhi viwango vya utoaji huduma. 
Ummy alisema  yupo tayari kuvibaini vyuo vya aina hiyo kwa kushirikiana na baraza la mitihani nchini NACTE na vitakavyobainika havistahili vifungwe kwani vinafanya udanganyifu na kushusha taaluma hiyo.
Alisema serikali iko tayari kuvitembelea vyuo vya uuguzi nchini na endapo vipo ambavyo vitaonekana kuwa havikidhi viwango vya utoaji elimu hiyo vitatakiwa viwajibishwe.

“Baraza la uuguzi mmefanya kazi muhimu ya ujenzi wa kituo hiki hivyo msikubali kuona baadhi ya watu wanawaharibia sifa,mkiona kuna mtu anaharibu kazi ni vyama mkamtaja kuliko kuchafuliwa na wachache ambao hawazingatii maadili,” alisema Ummy.

Akizungumzia suala la upungufu wa wauguzi ,alisema ufinyu wa bajeti ni moja ya chanzo kinachochangia  upungufu huo.
Ummy alisema lakini serikali inatambua na kuthamini majukumu ya wauguzi nchini .
Msajili wa baraza la wauguzi Lena Mfalila alisema ujenzi huo wa jengo hilo la kisasa unatarajia kutumia gharama za sh. bil 2.1 na utakamilika Januari mwaka 2017.
Alisema fedha za ujenzi huo zimetokana na ada ya uwanachama ya baraza hilo la wauguzi na wakunga. 
Mfalila aliomba serikali isaidie katika kukamilisha ujenzi huo ambapo mbali ya fedha walizotumia pia fedha nyingine bado zinahitajika.
Alibainisha kwamba baraza hilo ambalo lilianzishwa mwaka 1953 lilikuwa na lengo la kuhakikisha huduma zinatolewa salama na kwa viwango, kusimamia utendaji na kuwaendeleza kitaaluma wauguzi na kuwachukulia wanaokwenda kinyume cha maadili.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani alisema endapo baraza hilo litasimamia kikamilifu maadili ya wauguzi itasaidia kupunguza vifo vya akinamama na watoto ambao wamekuwa wakipoteza maisha wakati wa kujifungua.
Assumpter alisema pia baraza hilo litawezesha kufikia malengo ya kupunguza vifo ifikapo mwaka 2020.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania