CURRENT NEWS

Friday, December 23, 2016

ALIYEPOFUKA MACHO KUTOKANA NA FANSIDAR AOMBA MSAADA KWA MAGUFULI,WIZARA YA AFYA NA WATANZANIA

 MBGUNGE wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa,akizungumza jambo na mke wa Selemani Mgoto,baada ya kwenda kumjulia hali Mgoto,ambae anaomba msaada wa kupelekwa nchini India kupatiwa matibabu ya macho baada ya kupofuka kutokana na kumeza dawa zilizokwisha muda wake aina ya fansidar.(picha na Mwamvua Mwinyi)
 MKAZI wa Mlandizi,Kibaha Vijijini mkoani Pwani, Selemani Mgoto ,wa kwanza kulia kwenye kochi,akizungumza baada ya kwenda kutembelewa na mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaa (picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKAZI wa Mlandizi,Kibaha Vijijini mkoani Pwani, Selemani Mgoto (42)ameiomba serikali kupitia wizara ya afya ,kumsaidia kumpelekea nchini India kwenye matibabu ya macho ambayo ameyapoteza baada ya kutumia vidonge ya malaria (fansidar).
Amesema kinachomuumiza ni kuthibitishiwa na madaktari bingwa wa hospitali ya CCBRT na Muhimbili kuwa endapo ataenda India atapona lakini kinachomkwamisha ni sh.mil.18 kwa ajili ya safari hiyo.
Aidha kufuatia tukio hilo,mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini,Hamoud Jumaa amefanya jitihada za kuzungumza na mh January Makamba ambae amechangia sh.500,000 na kampuni make one ambayo imechangia mil.mbili.
Akizungumzia wakati alipokwenda kutembelewa na mbunge huyo ,nyumbani kwake kitongoji cha Janga,alisema tangu yamkute maswaibu hayo ni miaka minne sasa.
Mgoto alimuomba msaada rais John Magufuli kumtupia macho kwani nae ni kati ya wananchi wanyonge wasio na uwezo.
Hata hivyo alimwangukia pia waziri wa afya Ummy Mwalimu na naibu wake kuangalia uwezekano wa kumpeleka kwenye matibabu ya macho nchini India baada ya kuthibitishiwa kwamba anaweza kupona kama atapata matibabu zaidi.
Mgoto alisema hadi sasa ameshasaidiwa kiasi cha sh.mil.5 pekee hivyo bado kiasi kikubwa cha fedha ambacho kinahitajika kuondoka kwenda kwenye matibabu.
“Kweli kabla hujafa hujaumbika,namshukuru mungu kwa hili,nateseka,muda unazidi kwenda nahofia kupoteza macho yangu kabisa,watanzania wenzangu,mawaziri,wabunge na mh.rais wangu naomba mnisaidie nikaangalie nguvu za mungu”aliongea kwa uchungu.
Alieleza kuwa mnamo agosti 2012 alikuwa anaumwa na kwenda kupimwa malaria katika kituo cha afya cha Mlandizi ambapo aligundulika kuwa na wadudu 9 wa ugonjwa wa malaria.
Mgoto alisema aliandikiwa dawa aina ya fansidar na kuamua kwenda kuzinunua katika moja ya duka la dawa na baada ya siku mbili kuzimeza hali ilibadilika kutokana na sumu kali iliyokuwepo mwilini mwake  .
“Nilianza kuharibika kucha zangu za miguu na mikono,nilianza kutoka nywele zangu za kichwani,na kukimbizwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani,(Tumbi) kupata matibabu,na kugundulika dawa nilizomeza zilikuwa zimeisha muda wake”aliongeza.

Mgoto alisema mara ya mwisho alikwenda kuwaona madaktari bingwa wa hospitari ya CCBRT ya jijini Dar es salaam na muhimbili ambao walimwambia hawezi kupona Tanzania hadi aende nchini India .

Akizungumzia kuhusu maisha yake ,alieleza anashindwa kulipa kodi ya nyumba kwani amepanga anadaiwa kodi sh.300,000 huku kipato kikididimia kutokana na kutokuwa na uwezo tena wa kufanya kazi.
Nae mkewe mama Baraka,alisema maisha yao yamekuwa magumu ,kufuatia tangu mumewe apate matatizo hayo yeye alikuwa mjamzito.
Alisema kwasasa anajishughulisha na masuala ya salun ya kike na kumhudumia mumewe na watoto wao watatu .
Walimshukuru mbunge wao, kwenda kuwafariji na kuonyesha jitihada za kutaka kuwasaidia ili kutekeleza maombi ya wataalamu wa kiafya.
Kwa upande wake mbunge wa Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaa alisema hali ya mgoto hasa kimaisha sio nzuri.

Alisema inasikitisha kilichomuumiza ni dawa zinazoingizwa hapa nchini na wauzaji wengine kutofuata masharti ya kitaalamu hatimae kuwaingiza kwenye athari wasio na hatia.
Jumaa alisema ameshachukua hatua mbalimbali za kuongea na wadau ambapo January Makamba amechangia laki tano na mkurugenzi wa kampuni ya make one amechangia mil.mbili.
Alieleza anaendelea na jitihada nyingine za kwenda wizara ya afya na kuzungumza na wabunge wenzake ili kuangalia namna ya kumsaidia.
Jumaa aliwaomba wadau wa Kibaha ,mkoa wa Pwani na nje ya mkoa wajitokeze kumsaidia Mgoto aweze kwenda kutibiwa kwani kutoa ni moyo na sio utajiri.
Mtu yoyote anaehitaji kumsaidia mchango wake kwa hali na mali Seleman Mgoto ,atumie namba ya tigo pesa -0655-413939 au M-PESA 0754-413939 na akaunti namba NMB -80110000915.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania