CURRENT NEWS

Monday, December 5, 2016

DC BAGAMOYO AGEUKA MBOGO

Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Bagamoyo, alhaji Majid Mwanga ameagiza kukamatwa kwa aliyekuwa afisa ardhi wa wilaya hiyo Patrick Tsetse kwa tuhuma zinazodaiwa kufanya ufisadi katika malipo ya fidia za wakazi wa kijiji cha Pande na Mlingotini ili kupisha ujenzi wa Bandari.
Aidha mwenyekiti huyo ambae pia ni mkuu wa wilaya hiyo, ameagiza kukamatwa kwa wenyeviti wa vitongoji vitatu ambao wanasadikiwa kuhusika na tuhuma hizo.
Akizungumza na wakazi wa mlingotini na Pande wilayani humo,alhaj Mwanga alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kukamilika kwa uchunguzi uliofanywa na vyombo vya dola kufuatiwa kuwapo kwa malalamiko ya wakazi wa maeneo hayo.
Alisema baadhi ya wananchi hao walilalamika kupunjwa malipo yao wakati wa zoezi la ulipwaji wa fidia.
“Baada ya uchunguzi wa serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama tumebaini ufisadi mkubwa katika suala zima la ulipwaji wa fidia kwa wakazi hao "
" Uchunguzi huo umebaini kuwa hawa wenyeviti wenu wa vitongoji wameshiriki kwa namna moja ama nyingine katika kufanya ufisadi huo kwa kushirikiana na aliyekuwa mthamini wa mradi Patrick Tsetse "alisema alhaj Mwanga.
Alhaj Mwanga, alimuagiza OCD kuwachukua viongozi hao ili wakaisaidie polisi.
Hata hivyo aliwataja wenyeviti wa vitongoji wanaohusika na ubadhilifu huo kuwa ni mwenyekiti wa kitongoji cha Kikonga, Mgunda Dharau na kitongoji cha Kasiki, Ubezi Kondo. 
Mwingine ni wa kitongoji cha Mbegani, Jafari Hamis ambapo kuanzia sasa watachaguliwa wenyeviti wengine watakaojaza nafasi hizo.
Alieleza kwamba tume iliyoundwa ilibaini pia baadhi ya wananchi waliolipwa fidia kutumia picha za uongo za majengo na kupiga picha katika maeneo yasiyo yao ili kuweza kujipatia fedha.
“Kuna watu 11 wamelipwa jumla ya sh. mil. 9 kufidiwa mazao katika shamba ambalo si lao, na kuna mtu amelipwa sh. Mil 120 wakati hana hata eneo kwa hili kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe”alisema.
Akizungumzia kuhusiana na zoezi la tathmini kurudiwa ,alhaj Mwanga aliwataka wakazi husika kijiji cha Pande kujitokeza ili kuweza kufanyiwa tathmini upya.
Kuhusu eneo jipya ambalo wakazi hao wanapaswa kuhamishiwa ,alisema kuwa serikali ipo tayari kupima na kujenga miundombinu katika eneo hilo na kuwakabidhi wakazi wa Pande na Mlingotini.
Mkuu huyo wa wilaya alisema changamoto kubwa iliyopo katika eneno hilo ni ukubwa wa eneo  na pia kuna madai kuwa sehemu ya eneo hilo yenye ekari 221 kati ya 732 zimeshalipwa fidia  ilihali haijulikani nani aliyelipwa fidia hiyo.
Katika hatua nyingine mwenyekiti wa kitongoji cha Mkunguni Bozi Akili anadaiwa alijinyonga baada ya kuhojiwa na kamati.
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, dk Shukuru Kawambwa alisema uamuzi huo wa serikali wa kuamuru kuwapo kwa tathmini mpya kwa wakazi hao ni mzuri na hekima.
Alisema serikali imeahidi ushirikiano na kuhakikisha kila mkazi wa Pande na Mlingotini ambaye amepitiwa na mradi huo ananufaika.
Mwisho 
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania