CURRENT NEWS

Wednesday, December 28, 2016

JAFO AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA WILAYA MANYONI MKOANI SINGIDA


 Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo akipata maelezo toka kwa Agnesi Katumbo juu ya kusitishwa kwa kutolewa kwa risiti za kielectroniki ambayo ni kinyume na utaratibu wa Serikali na kutoa wiki moja kurudisha huduma hiyo ambayo ni chanzo cha kupotea kwa fedha za Serikali.Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo akisisitiza jambo kwa Wakuu wa Idara na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Manyoni (hawapo pichani) juu ya uwajibikaji kwa vitendo na sio kwa mazoea ili kuleta ufanisi sehemu za kazi walio kaa kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya Manyoni Geoffrey Mwambe, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Manyoni Moses Matonya na  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manyoni Edward Fussi.


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Selemani Jafo akimpima uzito mmoja wa watoto katika hospitali ya wilaya ya Manyoni alipotembelea hospitali hiyo wilayani manyoni leo hii.


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo akiangalia kitanda ambacho kinatumiwa na akina mama wajawazito wakati wa kujifungua katika Hospitali ya wilaya ya Itigi mkoani singida wakati alipofanya ziara ya kushtukiza. Kulia kwake ni Dkt. Mary Rume Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Itigi na anayefuatia ni Mkuu wa wilaya Manyoni Geoffrey Mwambe.     ...............................................................................................


NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amefanya ziara kushtukiza katika halmashauri mpya ya Itigi na Manyoni huku akibaini uwepo wa changamoto mbalimbali hususan upungufu wa dawa katika Kituo cha Afya Itigi na Hospitali ya wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

Akizungumza katika ziara hiyo, Jafo amesema mara baada ya kutembelea Halmashauri hizo amebaini changamoto za dawa katika kituo cha afya Itigi pamoja na vifaa katika chumba cha mama huku akisema zipo changamoto ambazo zinazotakiwa kutatuliwa ndani ya halmashauri hiyo.

Jafo akizungumza kuhusu suala la upatikanaji wa dawa, amesema tatizo hilo linaonekana ni kikwazo kutokana na watendaji kushindwa kutumia fedha za dharura wanazopewa na serikali kununulia dawa na vifaa tiba.

“Naziagiza Halmashauri hizi kuhakikisha zinaweka kipaumbele uboreshaji wa vituo vya afya kwa kununua dawa nyingi na vifaa vingine tofauti na kusubiri zinazotoka Bohari ya Madawa (MSD),”amesema Naibu Waziri huyo


Amewaagiza watendaji wa idara mbalimbali kuhakikisha wanashirikiana na mkurugenzi wa Itigi ili kutimiza wajibu wao na kuifanya halmashauri hiyo kuwa bora na kuwaonya kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

“Kila mtumishi ahakikishe anajali muda wa kazi na kuacha tabia ya kutoenda kwa ratiba ya kazi, watumishi wa Tamisemi wanatakiwa kujiamini katika kazi zao na kuacha uoga ama kufanya kazi hadi pale wanapofuatiliwa hasa kwenye miradi mbalimbali,”amesema 

Kadhalika, Naibu Waziri huyo amewataka wahasibu kuacha tabia ya kuabudiwa kutokana na kuamua kuidhinisha fedha hadi pale watakapojisikia na kusababisha miradi mingi kukwama na mingine kufa.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya ya Manyoni, Dk. Francis Mwanisa, amesema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa dawa licha ya kupokea wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali nje ya wilaya hiyo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania