CURRENT NEWS

Tuesday, December 20, 2016

JUMAA AUNGANA NA WAKAZI WA KIJIJI CHA BOKO KUANZA UJENZI WA MAABARA YA ZAHANATI
MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini,Hamoud Jumaa ,akishirikiana na wakazi wa kijiji cha Boko kata ya Boko,kufyatua matofali ili kuanza ujenzi wa maabara ya zahanati itakayosaidia kuondokana na tatizo la kukosa huduma ya vipimo kwenye zahanati hiyo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini,mkoani Pwani,Hamoud Jumaa ,ameungana na wakazi wa kijiji cha Boko kata ya Boko,kuanza ujenzi wa maabara ya zahanati itakayosaidia kuondokana na tatizo la kukosa huduma ya vipimo mbalimbali vya kiafya.
Aidha mbunge huyo amekamilisha ziara yake ya mwezi mmoja jimboni humo,ambayo ilikuwa na lengo la kushukuru na kusikiliza kero za wananchi.
Jumaa alisema ziara hiyo ni ya kawaida ambapo ametembelea kata 14 ,vijiji 26 na vitongoji 104 vilivyopo jimboni hapo.
Alieleza kuwa huwa akifanya ziara ya aina hiyo mara kwa mara arejeapo bungeni na sasa ameanza utekelezaji wa yale aliyoyabaini na kufikishiwa na wananchi .
Akizungumzia matokeo ya ziara yake,Jumaa alisema kwasasa ameanza utekelezaji wa kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara katika zahanati ya Boko,hali iliyosababisha kuhamasisha nguvu kazi ya jamii.
“Hadi kukamilika kwa maabara hii inahitajika zaidi ya mil.70 ,hivyo wakati napita kwenye ziara yangu kijijini hapa,walinieleza wananachi wameshachangishana fedha na kununua mifuko ya saruji 50 na mimi nikaamua kuwachangia malori ya mchanga”alisema Jumaa.
Alifafanua kwamba hamasa iliyopo baina ya wananchi hao inaleta faraja kwani katika mifuko na mchanga huo wamefyatua matofali 1,500 ambayo wataanza kujengea msingi na kupandisha jengo .
Jumaa alisema kikubwa anachosisitiza ndani ya jamii ni kuondokana na tabia ya kusubiri kila kitu kifanywe na serikali na ndipo alipoanzisha kauli mbiu ya “SISI KWANZA SERIKALI BAADAE”.
Aliwataka wananchi kushiriki kuchangia kwenye shughuli za kimaendeleo kama ilivyo katika sherehe na ngoma ili kupiga hatua ya maendeleo
Jumaa aliutaka uongozi wa kijiji kuongeza nguvu ya kuhamasisha wananchi waendelee kujitolea kuchangia na kujitoa kwenye nguvu kazi ili kuanza msingi na kukamilisha ujenzi haraka.

Kabla ya uhamasishaji wa kufyatua matofali wa maabara hiyo,ulitanguliwa na uwekwaji uzio kwenye lambo la maji kwenye kitongoji cha Waya kijiji cha Kwala.


Nae kaimu mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kibaha,Grace Boniface ,alisema ukosefu wa maabara unapelekea adha ya wagonjwa kufuata vipimo katika kituo cha afya Mkoani na hospitali ya mkoa ya Tumbi.
Alisema hiyo ni kero kubwa pamoja na tatizo la umeme ambapo kwasasa zahanati hiyo inatumia nishati ya umeme wa nguvu ya jua.
Grace aliwaomba wadau wa maendeleo na wa kiafya kujitolea kuwasaidia vifaa mbalimbali vya ujenzi vitakavyowezesha kukamilisha ujenzi huo.

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania