CURRENT NEWS

Thursday, December 15, 2016

MADEREVA 44 WAKAMATWA PWANI HUKU SABA WAKITARAJIWA KUFIKISHWA MAHAKAMANI


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MADEREVA wa mabasi ya abiria yaendayo mikoani wapatao 44 ,wamekamatwa na askari wa usalama barabarani mkoani Pwani,kutokana na makosa mbalimbali ya barabarani.


Sambamba na hilo,kitengo cha usalama barabarani mkoani hapo,kimetoa onyo  kwa baadhi ya madereva wenye tabia ya kutoa lugha chafu na kuwatishia askari wa usalama barabarani pindi wanapokamatwa na kutakiwa kulipia faini.

Kaimu kamanda wa usalama barabarani mkoani hapo,mrakibu wa  polisi ASP Salumu Morimori ,alisema madereva hao wamekamatwa kufuatia ukaguzi maalum unaofanywa katika barabara kuu Chalinze -Segera na Dar es saalam -Morogoro.
Alieleza kwamba zoezi hilo ni  endelevu likiwa na lengo la  kuzuia ajali hasa  katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa  mwaka.

"Tumejipanga kuhakikisha tunapunguza na kudhibiti ajali mkoani Pwani,tunachofanya ni kuwakamata wale wenye makosa na wengine kuwatoza faini na kuwafikisha mahakamani madereva watakaokutwa na makosa hatarishi ikiwemo ulevi, kuzidisha abiria, mwendokasi ", alisema Morimori .


Kamanda Morimori alieleza ,zoezi hilo  lilianza barabara  ya kwenda Kusini ambayo ni  mkoa wa  kipolisi Temeke kwa kushirikiana na wilaya ya Mkuranga  Pwani.
Alisema zoezi hilo  limeendelea katika barabara  ya Morogoro, ambayo ni kutoka Kibaha hadi Bwawani  mpakani mwa Pwani  na Morogoro,  na Chalinze  hadi  Manga mpaka wa Tanga na Pwani.

Alifafanua, madereva hao 44 walikamatwa siku moja pekee ambapo kati yao madereva 37 walitozwa faini za papo kwa papo  na madereva saba ambao waliokutwa na makosa hatarishi wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.


Hata hivyo,kamanda Morimori alitoa onyo  kwa baadhi ya madereva wenye tabia ya kutoa lugha chafu na kuwatishia askari wa usalama barabarani pindi wanapokutwa na makosa na kutakiwa kutozwa faini.

Alisema endapo dereva  ana malalamiko ni  vizuri akafuata taratibu kwani viko vitengo maalumu vya kushughulikia malalamiko na huko ndiko dereva   atakwenda kupata haki badala ya kutumia lugha za udhalilishaji kwa askari polisi.

Kamanda huyo alisema  ili dereva awe  salama barabarani anatakiwa kutii sheria bila shuruti kwa kuendesha kwa kuzingatia alama za barabarani.


"Hakuna haja ya kufikishana mahakamani, ili uwe salama barabarani ni fuata sheria za usalama barabarani, nakemea wale wenye tabia  ya kuwatolea lugha chafu askari , waache mara moja, hatuweza kuvumilia  vitendo hivyo"alisisitiza.
Kamanda Morimori ,alisema askari yuko  kwa mujibu wa sheria, kama kuna tuhuma dhidi ya askari ,sheria na taratibu zipo na zitafuata mkondo wake.

Mwisho.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania