CURRENT NEWS

Sunday, December 25, 2016

MBUNGE JUMAA AKABIDHI VITI VYA KUBEBEA WAGONJWA KITUO CHA AFYA MLANDIZI

Katibu wa mbunge wa jimbo la  Kibaha Vijijini ,Roytina Kishe akimkabidhi ,mganga mfawidhi wa kituo cha afya  cha Mlandizi,dokta  Mpola  Tamambele , viti vya kubebea wagonjwa 18 vilivyogharimu mil.5.4 kwa niaba ya mbunge huyo Hamoud Jumaa.(picha na Mwamvua Mwinyi)

 

Muuguzi kitengo cha wodi ya uzazi,katika kituo cha afya cha Mlandizi,Retistuta Eponda,(anaesukuma kiti),akijaribu kutumia kimoja ya kiti cha kubebea wagonjwa ambapo vimekabidhiwa viti 18 kituoni hapo na katibu wa mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijni,Roytina Kishe,kwa niaba ya mbunge Hamoud Jumaa.(Picha na Mwamvua Mwinyi),
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha Vijijini

MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini,mkoani Pwani,Hamoud Jumaa,ametoa msaada wa viti 18 vya kubebea wagonjwa ,vilivyogharimu kiasi cha sh.mil 5.4,katika kituo cha afya cha Mlandizi ili kuondoa adha ya uhaba wa viti hivyo uliokuwepo awali.

Aidha amesema baadhi ya viti hivyo vitagawanywa katika zahanati zilizopo pembezoni mwa mji huo ambazo zina upungufu huo .
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Jumaa katinu wa mbunge huyo,Roytina Kishe,alisema walitembelea kituo hicho na kubaini kuwepo kwa upungufu wa viti vya kubebea wagonjwa hasa wodi ya uzazi.
Alieleza kwamba Jumaa ametoa msaada huo kwa fedha zake mwenyewe ambapo hivi karibuni pia alisaidia vifaa tiba na mashine za kupimia magonjwa mbalimbali vilivyogharimu mil.11 katika kituo hicho.
Roytina alisema msaada huo utasaidia kuimarisha huduma zinazotolewa kituo cha afya Mlandizi na kupunguza changamoto ya upungufu uliokuwepo .
“Nakukabidhi, mganga mfawidhi wa kituo hiki viti hivi kwa niaba ya mbunge wa jimbo hili,ameomba mvitumie vizuri hasa kwa akinamama wajawazito na wanaokwenda kujifungua ambao ndio wanapata adha kubwa”alisema Roytina.
Alisema wakati Jumaa akiwa katika ziara yake ,alijionea changamoto kubwa hizo za ukosefu wa mashine za kupimia magonjwa ya kisukari,presha,vifaa tiba na viti vya kubebea wagonjwa.
Hata hivyo ,alisema mbunge huyo amejipanga kwenda kutatua kero ya ukosefu wa uzio hali inayosababisha watu kupita ndani ya kituo na kupelekea usumbufu kwa wagonjwa na kununua tanki la maji litakalogharimi kiasi chash.mil tano.
Roytina alisema suala hilo wanalisimamia kwa nguvu zote na limeshafikishwa wilaya,mkoa na ngazi nyingine likishughulikiwa ili adhma hiyo ifikie.


Alisema Jumaa amejipanga kuendelea kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo katika sekta ya afya,maji,elimu na kusaidia makundi maalum ikiwemo vijana,walemavu ,wanawake na wazee.

Alimuomba mganga mfawidhi kituoni hapo,kutunza vifaa vinavyotolewa na serikali pia wadau ambao wanashiriki kuunga mkono juhudi za serikali kukabiliana na changamoto za sekta ya afya kwani vinagharimu fedha nyingi.


Akipokea msaada huo,mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi,dokta Mpola Tamambele ,alimshukuru mbunge wa KIbaha Vijijini kwa niaba ya mganga mkuu wa wilaya ya Kibaha.


Alisema amepokea viti vya kubebea wagonjwa 18 vyenye magurudumu manne ambapo watatumia kituoni na nyingine watazipelekea katika zahanati zilizopo jimboni hapa.

Dokta Tamambele allisema awali kulikuwa na upungufu mkubwa wa viti vya kubebea wagonjwa,vifaa tiba na mashine za kupimia magonjwa  ya kisukari na presha.

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania