CURRENT NEWS

Tuesday, December 6, 2016

MBUNGE WA RUFUJI ALAANI VIONGOZI KUKWAMISHA MAENDELEO


ZIARA ya Mbunge wa Rufiji,Mohamed Mchengerwa,(CCM) imebaini uuzwaji wa ardhi iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya kiwanda cha sukari katika kijiji cha Chumbi ambayo imeuzwa kwa hekari moja shilingi 10,000.

Baada ya Mbunge huyo kufika katika mkutano wa hadhara wa kushukuru wananchi na kusikiliza kero zao juzi katika kijiji cha Chumbi alikutana na kilio cha eneo lenye ekari 2400 kuuzwa kwa shilingi milioni 24 pekee.

Wananchi wa eneo hilo walimtaja Diwani wa Kata ya Chumbi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Chumbi C,Salum Mtimbuko (CCM) kuwa ndiye aliyeuza eneo hilo kwa muwekezaji ambaye anamjua mwenyewe na alipewa Baraka zote na Mkuu wa Wilaya hiyo Juma Njwayo.


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapo,Mussa Mngeresa,ndiye aliyeeleza jambo hilo huku akishangiliwa na wananchi akimtaka mbunge huyo kumpeleka Mkuu wa Mkoa huo,Mhandisi Evarist Ndikilo,ili atatue kero hiyo kwani Njwayo ameshindwa.
‘’Uuzwaji huu ulifanywa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Chumbi C ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Chumbi ,Salum Mtimbuko (CCM)  na alipata Baraka kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji,Juma Njwayo,ambaye wananchi walimueleza suala hilo kabla lakini hakulifanyia kazi na kuwataka waache majungu’’alisema

Alisema viongozi hao wamewaudhi wananchi kwa kuuza ardhi kwa muwekezaji ambaye wanamjua wenyewe na kwamba ukifanyika uchaguzi wakati wowote kabla masuala hayo hayajataftiwa ufumbuzi CCM itapoteza nafasi hivyo kumuomba Mbunge huyo kufanya jitihada za kuwaleta viongozi wa mkoa,Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Akizungumzia suala hilo Mchengerwa alilaani kitendo cha viongozi hao kutaka kukwamisha maendeleo ya viwanda jimboni hapo kwani alishazungumza na Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji,Charles Mwijage,kuhusu ujenzi wa kiwanda cha sukari katika eneo hilo ambalo kwa sasa wananchi wamesema halipo.

‘’Jamani huku ni kurudishana nyuma na kutotambua juhudi za serikali na tunaowatetea haiwezekani viongozi wahusike kuuza ardhi ya kiwanda,wananchi tusikubali,sheria inaruhusu kuongea upya  na muwekezaji huyo ili atuachie ardhi yetu au aongeze fedha tukatafute eneo linguine,kuuza shilingi 10,000 ekari moja ni aibu’’
Akijibu tuhuma hizo diwani huyo alisema’’Nyie mnanionea wivu,wengine nimewasadia sana kuwalisha na familia zenu alafu mnanisema hapa,au kwasababu mnaniona naishi vizuri na wake zangu wawili na nina nyumba na magari? Pumbavu’’

Hata hivyo majibu ya diwani hiyo yalizua tafrani kwa wananchi kumzoea na kumtaka Mchengerwa arudi kwa mara nyingine na Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Mhandisi Evarist Ndikilo,Ili aweze kutatua kero zilizopo kwani viongozi wanauza maeneo kiholela na wanaposhitaki wa Mkuu wa Wilaya anakuwa upande wa wauzaji ardhi.

Mchengerwa aliwaleza wananchi hao kwamba ameshawasiliana na Mhandisi Ndikilo ,kuahidi kufanya ziara katika maeneo hayo Desemba 5 mwaka huu .

Mwisho. 

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania