CURRENT NEWS

Thursday, December 15, 2016

MWANANCHI MMOJA KATI YA WATANO (ASILIMIA 22) ANA HUDUMA YA KIBENKI

 
Mwananchi mmoja kati ya watano yaani asilimia 22; ana akaunti benki yake mwenyewe au ya ushirika na mtu mwingine. Hili ni ongezeko la asilimia 19 kutoka ilivyokuwa mwaka 2014. Umiliki wa akaunti za benki unatofautiana katika ya makundi mbalimbali: kaya tajiri asilimia 56; kaya masikini asilimia 6; wananchi wa mjini asilimia 41; wananchi wa vijijini asilimia 13; wanaume asilimia 24, na wanawake asilimia 20.

Miongoni mwa wale wasio na akaunti benki (asilimia 78), nane kati ya kumi wanataja kutokuwa na fedha kama sababu kuu ya kutokuwa na akaunti benki.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kupitia muhtasari wake uitwao Fedha, fedha, fedha! Wananchi na huduma rasmi za kifedha. Muhtasari huo unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,800 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 14 na 26 septemba 2016.

Idadi ya watu wazima wanaotumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi imeongezeka kutoka asilimia 61 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2016. Hii inamaanisha kwamba lengo la Serikari la kufikisha huduma za kifedha kwa asilimia 50 ya watanzania ifikapo mwaka 2016 limepitwa kwa kiasi kikubwa. Hii imepelekea serikari kujiwekea Lengo jipya la kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2017. Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania idadi ya watanzania waliokuwa wamefikiwa na huduma na kifedha kupitia simu za mkononi ilikuwa asilimia 50 mwaka 2014 hivyo basi utafiti huu wa Sauti za Wananchi umeonesha kwamba kuongezeka kwa idadi ya waliofikiwa na huduma hizi ni dalili njema.

Hata hivyo ifahamike kuwa wahojiwa wa Sauti za Wananchi hupewa simu za mkononi ili kufanikisha zoezi la kupata takwimu sahihi zisizo na ubaguzi.

Asilimia 79 ya watumiaji wa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu wanasema wanaridhishwa na huduma zinazotolewa. Ni mtumiaji mmoja tu kati ya kumi (asilimia 10) anayesema haridhishwi na huduma hizo. Karibu wote waliosema hawaridhishwi na huduma, wametaja gharama kubwa kama sababu kuu ya kutokuridhishwa kwao. Wananchi  walipoulizwa kuhusu suala la gharama za huduma za fedha kwenye mitandao ya simu za mikononi kwa ujumla, 4 kati ya 10 (asilimia 38) walisema gharama hizo ni kubwa mno.

Kutuma na  kupokea pesa ndio huduma maarufu zaidi kwa watumiaji wa huduma za fedha kupitia simu za mikononi (inatumiwa na asilimia 79 ya wananchi). Wananchi wachache hutumia huduma hizo kuweka akiba (asilimia 22) au kulipia huduma mbalimbali (asilimia 11).

Upatikanaji wa huduma nyingine za kifedha pia umekua nchini Tanzania, ingawa ni kwa kiwango kidogo ukilinganisha na huduma za fedha kwenye mitandao ya simu za mikononi.

Mwananchi mmoja kati ya watatu (asilimia 35) ameshawahi kukopa fedha. Kwa kiasi kikubwa mikopo hii (asilimia 41) ilitoka kwa ndugu au marafiki. Asilimia 31 ya Wananchi wanaripoti kukopa fedha kutoka kwenye vyanzo rasmi ikiwemo benki (asilimia 16), taasisi zinazotoa mikopo midogo midogo (asilimia 11) na vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (asilimia 4). Watanzania wengi wamekopa fedha kwa ajili ya biashara zao (asilimia 34) au kwa ajili ya matumizi ya kila siku (asilimia 26).

Mwananchi mmoja kati ya wanne (asilimia 27) ana huduma ya bima, wengi wao wakisema bima hiyo ni ya afya.

Kwa ujumla, mwananchi mtu mzima mmoja kati ya sita (asilimia 14) nchini Tanzania hajafikiwa na huduma za kifedha. Hii inamaanisha hana akaunti ya benki, akaunti kwenye mitandao ya simu za mikononi, bidhaa ya bima wala mkopo kutoka kwenye taasisi rasmi za kifedha (benki, taasisi zinazotoa mikopo midogo midogo au vyama vya ushirika vya akiba na mikopo). Viwango vya kutokufikiwa na huduma za kifedha vinatofautiana kati ya makundi mbalimbali kwenye jamii:

  • Wanaume: asilimia 12, wanawake: asilimia 16
  • Mijini: asilimia 7, vijijini: asilimia 18
  • Kaya tajiri: asilimia 2, kaya masikini: asilimia 24
  • Vijana miaka 18-29: asilimia 12, wazee zaidi ya miaka 50: asilimia 17

Mkurugenzi mtendaji wa Twaweza, Ndugu Aidan Eyakuze anasema, “Upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha kumeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini.  Upatikanaji wa mikopo na bima, uwezo wa kutuma na kupokea pesa kwa urahisi na usalama, na sehemu salama za kuweka akiba yoyote vinasaidia kupunguza ugumu wa maisha ya watu masikini na kuongeza uzalishaji wao.  Wakati huo huo, huduma rasmi za kifedha kwa sasa zinashikiliwa kwa kiwango kikubwa na mitandao ya simu za mikononi. Na takwimu zinaonyesha kuwa huduma hizi hutumika kwa kiasi kikubwa kutuma na kupokea fedha. Hii inamaanisha kuwa wananchi wengi hawafurahii ongezeko la huduma ikiwemo bima, upatikanaji wa mikopo na akiba. Ni wajibu wa makampuni ya mitandao ya simu za mikononi, benki na taasisi nyingine za kifedha kufanya kazi kwa pamoja na kutoa huduma zitakazowasaidia wale ambao hawajafikiwa na huduma hizi muhimu.”

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania