CURRENT NEWS

Thursday, December 8, 2016

TASAF PWANI YAZIONDOA KAYA 1,664 KATIKA MPANGO WA TASAF AWAMU YA III

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MFUKO wa maendeleo ya jamii (TASAF) mkoani Pwani ,umeziondoa kaya 1,664 ambazo hazikustahili kuingizwa katika mpango wa kunusuru kaya masikini awamu ya tatu na kuokoa sh.mil.80.989 ambazo zingetumia na kaya hizo.
Kaya hizo zimeondolewa katika mpango huo baada ya kufanyika uhakiki kwenye halmashauri mbalimbali mkoani hapo  ili kubaini kaya  zisizo na sifa ambazo ziliandikishwa .
Hayo yalisemwa na mratibu wa TASAF, mkoani Pwani,Asha Itelewe,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa kunusuru kaya masikini-TASAF awamu ya tatu kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita kuanzia julai 2015/juni 2016.
Alisema kaya hizo ziliingizwa kimakosa kwa kutofuata vigezo ambapo zisingegundulika ingesababisha hasara ya mamilioni ya fedha kutumika kwa watu wasio walengwa.
Asha alizitaja takwimu za kaya ambazo ziliingizwa kimakosa katika kila wilaya kuwa ni pamoja na wilaya ya Bagamoyo kaya 987, ambapo wameokoa mil.19.740,Mji wa Kibaha kaya 58 wameokoa mili.2.436,wilaya ya Kibaha 187 fedha mil.20 na Kisarawe 44 wameokoa mil.3.9.
Wilaya nyingine mi Mafia kaya 28 huku wakiokoa mil.806,Mkuranga kaya 224 na fedha zilizookolewa ni sh.mil.22.748 na Rufiji kaya 136 ambako wameokoa mil.11.356 .
Hata hivyo Asha alieleza kuwa katika kipindi hicho jumla ya kaya 33,937 na walengwa 101,059 wamenufaika na mpango huo na kutumia bil.1.87.
“Walengwa wa mpango ni kaya masikini zinazoishi katika mazingira duni na hatarishi,kaya hizo ziwe zenye kipato cha chini sana na si cha uhakika ukilinganisha na kaya nyingine kijijini au mtaani’
“Ambazo hazina uhakika wa kupata milo mitatu kwa siku,zina watoto ambao hawaendi shule au kuacha shule kutokana na kushindwa kumudu gharama na hawaendi kliniki kupata huduma kutokana na umaskini”alisema Asha.
Asha alisema wanafunzi wanaonufaika na mpango sule za msingi ni 25,650,shule za sekondari 2,965 na watoto chini ya miaka mitano ni 8,644.
Katika hatua nyingine Asha ,alisema wanakabiliwa na changamoto ya uwepo wa kaya nyingi maskini hazijafikiwa na mpango kufuatia upungufu wa raslimali fedha na ufinyu wa fedha za kufanya ufuatiliaji.
Awali akifungua kikao hicho ,mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,aliwataka waratibu wa TASAF mkoa na wilaya wawe makini na takwimu wanazozitoa juu ya matumizi ya fedha zinazotolewa kwenye mpango huo.
Alisema fedha inayotengwa kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini ni nyingi hivyo inapaswa kuwafikia walengwa wenye mahitaji na sio vinginevyo.
Mhandisi Ndikilo,aliwataka waratibu wa TASAF kutoka halmashauri za mkoa huo na mratibu wa mkoa,wafuatilie na kusimamia mpango huo kwa kuingiza watu wanaostahili .
Alisema mpango wowote unaotumia mabilioni ya fedha nchini ni lazima usimamiwe kwenye tathmini,takwimu na kufuatilia mpango ama mradi mzima bila ubabaishaji.
Mhandisi Ndikilo,alisema ni majukumu yao kusimamia mpango huo ipasavyo na endapo wapo watakaothibitika kuhusika kuvuruga utaratibu  ama kuwepo kwa udhaifu katika usimamizi wa utekelezaji wa mpango watachukuliwa hatua stahiki.
Mkurugenzi wa ukaguzi wa ndani kutoka TASAF makao makuu,Christopher Sanga,alisema mkoa huo bado unatakiwa kuongeza juhudi ya kusimamia miradi ya TASAF ili iwe yenye viwango stahili kulingana na fedha wanayotoa.
Sanga alisema miradi hasa ya miundombinu hairidhishi hivyo kuna kila sababu ya waratibu hao kusimamia kikamilifu ili kuhakikisha  miradi hiyo iendane na kiwango cha fedha na sio tathmini ya macho.

Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania