CURRENT NEWS

Wednesday, December 7, 2016

RC NDIKILO AYAKALIA KOONI MAKAMPUNI YASIYOLIPA MNADA WA KOROSHO PWANI

MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,akizungumza baada ya kubaini ubabaishaji unaofanywa na wakuu wa kampuni ya ALPHA CHOICE LTD na KAASAL COMMODITIES LTD kushindwa kulipa kwa wakati korosho za mnada wa mwaka huu mkoani hapo(Picha na Mwamvua Mwinyi).

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,ameliagiza jeshi la polisi mkoani humo,kuwakamata na kuwafungulia mashtaka wakuu wa kampuni za ALPHA CHOICE LTD na KAASAL COMMODITIES LTD .
Wakuu wa makampuni hayo wamejikuta wakipata mdharuba huo ,kutokana na kudaiwa kushindwa kulipa kwa wakati zaidi ya sh.bil 5.794 za mnada wa zao la korosho msimu huu.
Aidha amemuomba mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego kuzuia korosho zilizonunuliwa na makampuni hayo
hadi pale watakapolipia korosho walizonunua mkoani Pwani.
Mhandisi Evarist Ndikilo alilazimika kuchukua hatua hiyo kali kwa lengo la kukomesha tabia zinazofanywa na baadhi ya makampuni mbalimbali katika minada .

Hata hivyo alitoa msimamo huo ,baada ya kubainika kwa makampuni hayo  kuwa na nia ya kukataa kulipa fedha za korosho za wananchi wa mkoa wa Pwani.
Mhandisi Ndikilo alielezea kwamba fedha hizo zilitakiwa kulipwa baada ya kununua korosho katika mnada .
“Baada ya kugundua hila hizo za kutaka kutoroka bila kulipa  fedha hizo, awali niliamua kufanya kikao ambacho kiliwashirikisha bodi ya korosho Tanzania (CBT) ,chama cha ushirika mkoa wa Pwani (CORECU), Jeshi la Polisi na sekretarieti ya mkoa “alisema .

Mhandisi Ndikilo alifafanua kuwa kampuni ya ALPHA CHOICE LTD aliingia mkataba wa kununua tani 1,430.9 za korosho yenye thamani ya sh.bil 4,202,514,402 na kutakiwa kulipia 23 Novemba, 2016.
Akielezea makubaliano na kampuni ya KAASAL COMMODITIES LTD,alisema iliingia mkataba wa kununua tani 500.037 zenye thamani ya sh.bil 1,591,608,288.
Alisema kampuni hiyo ya KAASAL yenyewe ilitakiwa kulipa tarehe 16 Novemba 2016 lakini mpaka sasa hazijalipa fedha hizo na kukiuka makubaliano ya mkataba wa mnada huo .

Mhandisi Ndikilo alibainisha ,makampuni hayo yamevunja taratibu za makubaliono ya mnada ambapo zinamtaka mnunuzi akishinda zabuni aandae malipo ndani ya siku saba.
Ili kuwalazimisha wakuu wa kampuni hizo kulipa fedha hizo, mhandisi Ndikilo,amezuia korosho zote za msimu huu zilizonunuliwa na makampuni hayo ambazo wamelipia na bado hawajazichukua.
“Korosho hizo ziendelee kushikiliwa hadi watakapolipa fedha za wakulima,huu ni unyonyaji wa watu wanyonge ambao wanatumia nguvu nyingi kisha kuwalalia bila hatia”alielezea.
Katika hatua nyingine alilielekeza jeshi la polisi na wakuu wa wilaya  zote mkoa wa Pwani kusimamia zoezi la uzuiaji na utoaji wa korosho kwa kampuni hizo.
Sambamba na hilo ,aliomba mkuu wa Mkoa Mtwara, Halima Dendego ,aungane nae kupigania suala hilo kutetea wanyonge kwa kuzuia korosho zote zilizonunuliwa na makampuni hayo.
Mhandisi Ndikilo ,alieleza korosho hizo zilizonunuliwa mkoani Mtwara, tayari zipo bandarini kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi hivyo zizuiwe mpaka pale watakapolipia korosho walizoahidi mkoani Pwani.
Baadhi ya wadau wa kilimo cha zao la biashara la korosho mkoani hapo,akiwemo Tunduguru Naimo na Zubeda Isaya walipongeza hatua alizochukua mkuu wa mkoa huyo.
Walisema baadhi ya makampuni yamekuwa yakiwakandamiza wakulima hao huku wao wakinufaika .


 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania