CURRENT NEWS

Wednesday, December 28, 2016

RC NDIKILO-TASAF WABANENI WARATIBU WANAOTIA DOA MPANGO WA TASAF III


MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo, akizungumza jambo na waratibu mbalimbali wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) kutoka halmashauri za mkoani humo Pwani na baadhi ya watendaji wilaya na mkoa.(picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amepokea tuhuma kutoka kwa baadhi ya wananchi kuwa wamekuwa wakitishiwa kuondolewa katika mpango wa kunusuru kaya maskini awamu ya III(TASAF III)kutokana na kuuliza maswali mengi kuhusu fedha zao kwenye mikutano.

Aidha ameelezwa wapo baadhi ya walengwa wa mpango huo ambao wamekuwa wakipewa sh.20,000 badala ya sh.24,000  kwa madai ya baadhi ya waratibu kukosa chenchi.

Kufuatia malalamiko hayo ,mhandisi Ndikilo,ameitaka TASAF makao makuu na mratibu wa Tasaf Mkoani Pwani,Asha Itelewe kusimamia masuala hayo kwani yanapaka matope mpango huo.

Akizungumza na waratibu wa Tasaf kutoka halmashauri mbalimbali na baadhi ya watumishi wa idara za masuala ya jamii,aliwaambia wafuatilie,watafiti ili kupata ushahidi.

Mhandisi Ndikilo alisema haiwezekani kufumbia macho vitendo ambavyo vinaashiria kuchafua juhudi za serikali hivyo wafuatilie maeneo yanayogawa fedha kwa walengwa .

“Watu wa makao makuu ya Tasaf,mratibu wa mkoa malalamiko hayo nimefikishiwa ofisini kwangu,na vyombo mbalimbali na wananchi ,haina budi kuweka mezani ili kujisahihisha na kuvidhibiti vitendo hivi”

“Wanaambiwa mbona unauliza maswali mengi mengi kila wakati,,unataka kuwapa wengine ufahamu eeh hivyo kuamua kukaa kimya kwa kuhofia kuondolewa”alisisitiza mhandisi Ndikilo.

Alisema wananchi wana kila sababu ya kuachiwa huru kuuliza maswali ili kufahamu kuhusu mpango kiundani bila kubanwa wala kupewa adhabu ya kufumuliwa kwenye mpango.

Mhandisi Ndikilo,aliwataka waratibu wa wilaya kufanya kazi zao kikamilifu na kuwahudumia walengwa inavyotakiwa pasipo kufanya ubabaishaji wala kuwatishia watu wanaosimamia haki yao.  


Akizungumzia suala la kukatwa fedha za mpango kwa walengwa ,alisema waratibu ndio wanaojua maeneo ya kupata chenchi ikiwemo katika taasisi za kifedha na kuwa na fedha kamili na sio vinginevyo.


Mhandisi Ndikilo,aliwaomba kuacha kuwapa usumbufu na mzigo wananchi ambao wengi wao wapo maeneo ya vijijini.



Hata hivyo alimtaka mratibu wa Tasaf mkoa,kuonyesha tathmini za fedha zinazotumika na mchanganuo wa mchango wa wananchi katika mpango huo wa kijamii.

Nae mkurugenzi wa ukaguzi wa ndani kutoka TASAF makao makuu,Christopher Sanga,alisema wamepokea malalamiko hayo na yatafanyiwa kazi ili kubaini ukweli uliopo.
Alisema kama wapo waratibu wanaonyanyasa walengwa wa mpango huo ni lazima wabadilike na endapo yupo atakaebainika kufanya vitendo hivyo atawajibishwa.


Sanga alieleza kuwa wamefanya utafiti na ukaguzi ambapo wamegundua waratibu wengi hawatumii fedha inavyopaswa wakati zingetumika inavyotakiwa matokeo yake yangeleta ufanisi wa hali ya juu.


Aliwataka waratibu kuwa makini na uendeshaji wa mpango huo kwa kutumia fedha ipasavyo hasa kwenye miradi ya miundombinu na kila eneo linalotakiwa ili kunufaisha walengwa.

Kwa upande wake mratibu wa Tasaf mkoani Pwani,Asha Itelewe ,alipokea maagizo yote kutoka kwa mkuu wa mkoa huo na kusema atayashughulikia.


Jumla ya kaya 33,937 na walengwa 101,059 wamenufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini awamu ya III mkoani Pwani na kutumia sh.bil.1.87 huku kaya 1,664 zilizokuwa hazikustahili ziliondolewa .
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania