CURRENT NEWS

Wednesday, December 14, 2016

RPC PWANI - KATI YA WATUHUMIWA 10 WA MAKOSA YA KUBAKA/KULAWITI/MIMBA ZA WANAFUNZI NI MADEREVA BODABODA

Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Boniventure Mushongi,akikabidhi vizibao kwa baadhi ya madereva pikipiki(bodaboda)Mailmoja Kibaha baada ya kuzungumza nao kuhusiana na namna ya kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili,wa pili kutoka kushoto ni mkuu wa kitengo cha dawati la jinsia na watoto,Yusta Milinga .

Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Boniventure Mushongi,akizungumza jambo na baadhi ya madereva pikipiki(bodaboda)Mailmoja Kibaha, kuhusiana na namna ya kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili.(Picha na Mwamvua Mwinyi)


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

MADEREVA pikipiki(bodaboda) mkoani Pwani, wameaswa kuacha kujihusisha kwenye matukio mbalimbali ya ukatili ,ikiwemo ubakaji na kuwapa mimba wanafunzi wa kike., kwani takwimu inaonyesha kati ya watuhumiwa 10 wa makosa  hayo watuhumiwa watatu ni madereva bodaboda.

Aidha wametakiwa kuanzisha timu za ulinzi na usalama ili kujenga daraja katika kupeana elimu na kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Akitoa rai hiyo,kwa baadhi ya madereva pikipiki na wananchi Mailmoja,Kibaha,kamanda wa polisi mkoani Pwani,Boniventure Mushongi,alisema hakika hilo ni janga kubwa ambalo linahitaji kupaza sauti ili kukabiliana nalo.

Alieleza utafiti uliofanywa na dawati la jinsia na watoto ,mkoani hapo limebaini kwamba baadhi ya madereva bodaboda hujihusisha na vitendo hivyo jambo ambalo linahitajika kupigwa vita.

Kamanda Mushongi ,alisema madereva hao kijumla wasaidiane kuwafichua wale ambao wamekuwa wakiitia doa kazi hiyo na kuwachafua mbele ya uso wa jamii.

Anawataka kupitia umoja wao kupinga matendo yote ya ukatili na udhalilishaji sanjali na kuwalinda watoto ili kupambana dhidi ya vitendo vya ukatili kwa lengo la kupunguza na kutokomeza vitendo hivyo.

Kamanda Mushongi,alisema kuwa kijana au dereva bodaboda haimaanishi kufanya vitendo viovu ama kudhalilisha watu.

“Tumeona ipo haja ya kukutana na madereva wa pikipiki ambao wengi wenu wameonekana kuwa wanajihusisha kwa kiwango cha hali ya juu kwenye matukio ya kulawiti,kubaka,kushiriki matukio ya kiuhalifu na kutelekeza familia zenu”

“Takwimu zinaonyesha kila kwenye watuhumiwa 10 waliokamatwa kwa makosa mbalimbali ya ukatili watuhumiwa 3 ni madereva pikipiki”alisema kamanda Mushongi.

Hata hivyo kamanda Mushongi,aliwaomba wazazi kuhakikisha wanasimamia malezi ya watoto kwa karibu badala ya kuwaachia kina mama pekee ambao baadhi yao huwaachia wasichana wa kazi jukumu hilo .

Alifafanua kuwa tabia ya kuwaachia wasichana wa kazi pekee jukumu la kulea watoto huchangia mmomonyoko mkubwa wa maadili.

Kamanda Mushongi alisema utafiti huo pia unaonyesha hali ngumu ya maisha inachangia wazazi wengi kukosa muda wa kukaa na familia zao na kuzungumza kuhusu madhara ya mahusiano katika umri mdogo.

“Suala hilo hupelekea baadhi ya watoto kujitumbukiza katika vitendo vya ngono wakiwa katika umri usiofaa na kusababisha kupata ujauzito ama kuambukizwa magonjwa ya kuambukiza ikiwemo virusi vya ukimwi”alisema.

Makosa ya ukatili wa kubaka mkoani hapa,yameongezeka kutoka 257 kwa kipindi cha January hadi septemba 2015 na kufikia 310 kipindi kama hicho mwaka 2016 hivyo kuwa na ongezeko la makosa hayo 53.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania