CURRENT NEWS

Thursday, December 22, 2016

UHUSIANO KATIKA YA MATOKEO YA KUJIFUNZA NA UTAPIAMLO


Uhusiano ni mkubwa kati ya matokeo ya kujifunza na utapiamlo
Twaweza inatoa wito kwa wazazi na shule kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni

Dar es Salaam, 22 Desemba 2016: Takwimu mpya zilizotolewa na Uwezo (iliyopo Twaweza) zinaonesha uhusiano kati ya matokeo ya watoto ya kujifunza na utapiamlo.

Miongoni mwa watoto wenye miaka 10 mpaka 14:

Somo la Kingereza (uwezo wa kusoma hadithi ya kingereza ya kiwango cha darasa la 2):

  • Watoto wenye utapiamlo – asilimia 17.9 walifaulu
  • Watoto wenye utapiamlo wa wastani – asilimia 16.4 walifaulu
  • Watoto wasio na utapiamlo – asilimia 25.8 walifaulu

Somo la Kiswahili (uwezo wa kusoma hadithi ya Kiswahili ya kiwango cha darasa la 2):

  • Watoto wenye utapiamlo – asilimia 46.3 walifaulu
  • Watoto wenye utapiamlo wa wastani – asilimia 51.3 walifaulu
  • Watoto wasio na utapiamlo – asilimia 65.8 walifaulu

Somo la Hisabati (uwezo wa kufanya hesabu za kuzidisha za kiwango cha darasa la 2):

  • Watoto wenye utapiamlo – asilimia 35.5 walifaulu
  • Watoto wenye utapiamlo wa wastani – asilimia 37.7 walifaulu
  • Watoto wasio na utapiamlo – asilimia 53.4 walifaulu

Watoto wasio na utapiamlo wanafaulu zaidi kusoma masomo ya Kiswahili na Hisabati kuliko wale wenye utapiamlo.

Matokeo haya yametolewa na Uwezo (iliyopo Twaweza) katika halfa iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Halfa hiyo ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa semina za JiElimishe zinazofanyika kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu na Twaweza. Takwimu juu ya uhusiano kati ya lishe na matokeo ya kujifunza zilikusanywa kati ya Oktoba na Desemba 2015 kutoka kwa watoto 197,451 na kaya 68,588.

Takwimu zilizokusanywa zinaonesha kuwa, kwa ujumla kitaifa, asilimia 4 ya watoto wenye umri chini ya miaka 5, asilimia 5.6 ya watoto wenye miaka kati ya 5 na 9 na asilimia 5.7 ya watoto wenye miaka kati ya 10 hadi 14 wana utapiamlo.

Hatahivyo kuna utofauti mkubwa kiwilaya: asilimia 23.9 ya watoto wa Songea Mjini walio chini ya miaka 5 wana utapiamlo ukilinganisha na asilimia 0.3 wilaya ya Tabora Mjini na Musoma Mjini.

Kwa wastani, asilimia 50 ya kaya zinamudu milo mitatu kwa siku. Matokeo yanaonesha kuwa baadhi ya wilaya zina zaidi ya asilimia 85 ya kaya zinazomudu milo mitatu kwa siku (Mbulu asilimia 97.6, Kishapu – asilimia 88.2, Mafinga Mjini – asilimia 88, Tunduma asilimia 86.4, Moshi Mjini – asilimia 86). Ilihali katika wilaya nyingine, kaya chini ya asilimia 40 ndizo zinazomudu milo mitatu kwa siku (Masasi – asilimia 38.6, Tandahimba – asilimia 35.5, Mtwara Vijijini – asilimia 27.6, Nanyumbu – asilimia 23.1).

Kitaifa, ni shule moja tu kati ya tano inayotoa huduma ya chakula cha mchana shuleni (asilimia 23). Kwa mkoa wa Kilimanjaro, asilimia 79 ya shule zinatoa chakula cha mchana lakini katika mkoa wa Geita, ni asilimia 5 tu ya shule zinazomudu chakula cha mchana kwa watoto.

Meneja wa Uwezo Tanzania, Bi Zaida Mgalla, alisema “Takwimu hizi zinatupa taswira ya hali ya lishe ya watoto. Inaonekana wazi kwamba upo uhusiano mkubwa kati ya lishe ya watoto na matokeo yao ya kujifunza. Tayari tumeshajionea hali ya lishe ya watoto ina madhara kwenye kusoma Kingereza ukilinganisha na Kiswahili na Hisabati. Habari njema ni kwamba suala hili linaweza kujadiliwa, na watoto wanaweza kupatiwa chakula shuleni. Utoaji wa chakula shuleni inaweza ikawa njia mojawapo ya kuwapa motisha wanafunzi kuhudhuria zaidi shuleni.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze anasema, “Utafiti huu umethibitisha kile ambacho wengi wetu tulikuwa tunadhani: Uwezo wa watoto kufanya vizuri shuleni unaathiriwa na jinsi wanavyopata lishe nzuri. Katika awamu hii ya elimu bila malipo ya ada, suala la utoaji wa chakula shuleni limeachwa njia panda. Halijaainishwa kwenye fedha za ruzuku zinazotumwa moja kwa moja shuleni na serikali. Wazazi nao wameacha kutoa michango shuleni, kutokana na matamko rasmi ya kufuta michango yote mashuleni. Je, suala la michango ya wazazi kwa ajili ya chakula cha watoto wao waki shuleni bado halizungumziki? Si vibaya tukalijadili hili pia, miongoni mwa jitihada nyingine sinazofanywa kuhakikisha watoto wetu wanajifunza."

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania