CURRENT NEWS

Thursday, December 1, 2016

VIJIJI 26 JIMBO LA CHALINZE VYATESEKA NA JANGA LA NJAA

Diwani wa kata ya Lugoba, Rehema Mwene, akizungumza jambo katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Chalinze. (Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
WAKAZI wa vijiji 26 kati ya vijiji 68 ,vilivyopo jimbo la Chalinze ,wilaya ya Bagamoyo,bado wanateseka na janga la njaa hivyo wanahitaji msaada wa chakula ili kukabiliana na janga hilo .
Kufuatia hali hiyo madiwani wa halmashauri ya Chalinze ,wameiomba serikali kuwasaidia wananchi hao kwa kuzingatia vijiji ambavyo vina hali mbaya zaidi .
Wakizungumzia suala hilo kwa nyakati tofauti,akiwemo diwani wa kata ya Talawanda ,Saidi Zikatimu ,alisema awali katika tathmini ,waliiomba serikali tani 4,000 za msaada wa chakula lakini walipatiwa tani 200 pekee.
Alieleza kuwa  kati ya tani 200 za chakula cha msaada walichopokea tani 180 ni kwa ajili ya kugawanywa bure na tani 20 ni chakula cha kununua kwa wale wenye uwezo ambacho hakijatosheleza .
Alisema tani  zilizotolewa ni chache ukilinganisha na hali halisi ya tatizo hivyo kama serikali iliweza kuona umuhimu wa suala hilo kwa mara ya kwanza ,basi isaidie kumaliza msaada kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa.
Zikatimu ambae pia ni mwenyekiti wa halmashauri hiyo,aliishukuru serikali kwa kuzingatia maombi yao ya awali licha ya tatizo kubaki kuwa kubwa.
“Katika kata ambazo zimekosa ni kata ya Vigwaza,Bwilingu na Kiwangwa ambapo kata ya Msoga,Pera na Ubena zimepata kijiji kimoja kimoja na katika kata nyingine vijiji vilivyopo kwenye kata hizo vimepata vichache “alifafanua Zikatimu.
Alisema wananchi kwasasa wanalima lakini mazao sio msimu wake wa kuyavuna kwahiyo changamoto imebaki pale pale na hali ya kiuchumi ikiwa ni mbaya.
Nae diwani wa kata ya Kimange,Hussein Hading’oka ,alisema tatizo la njaa limekumba karibu kata nzima kutokana na mavuno kuwa sio ya kuridhisha miaka miwili mfululizo.
Alisema serikali ya wilaya na mkoa ilishughulikia suala hilo katika ngazi za juu pamoja na halmashauri iliomba chakula katika vikao mbalimbali lakini kilichopelekwa hakikuwafikia walengwa wote.
Hading’oka alieleza kwamba chakula cha msaada kimefikia vijiji vitatu kata ya Kimange huku vijiji viwili ikiwemo kijiji cha Pongwe Mnazi na Kikwazu vimekosa kabisa .
Awali diwani kata ya Kiwangwa,Malota Kwaga ,aliomba kuwepo kwa usimamizi mzuri wa kugawa chakula kinachotolewa na serikali kama msaada .
Alisema haiwezekani vikao vya madiwani vikiweka msimamo wa jambo kunatokea mtu mwingine ambae anayumbisha msimamo huo na kupeleka changamoto zisizo na tija.
Malota aliyasema hayo kutokana na kudai kwamba baada ya serikali kutoa tani hizo 200,kikao kilipanga utaratibu wa kugawa chakula hicho lakini alitokea afisa kilimo wa wilaya ambae hakuwashirikisha madiwani na kugawa chakula kiholela.
Diwani huyo wa Kiwangwa alisisitiza kuwa ,jambo hilo sio la masihala inatakiwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo afuatilie juu ya changamoto hiyo na ukiletwa msaada mwingine wa chakula afuate maagizo ya baraza.
Kwa upande wake ,kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze ,Isaack Kama alikiri kuwepo kwa changamoto ya kukabiliana na njaa katika baadhi ya vijiji .
Alisema halmashauri ilipokea tani 200 kati ya 4,000 zilizoombwa ,na kamati ya maafa wilaya ndio ambao wanatakiwa kukaa na kufuatilia chakula kinachogawiwa .
Isaack ,alisema kwasasa taarifa aliyonayo ni kwamba suala hilo linasimamiwa na idara ya kilimo na serikali wilaya na mkoa ili kuhakikisha chakula kingine kinaombwa ili serikali iweze kusaidia.
Mwisho  
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania