CURRENT NEWS

Wednesday, December 28, 2016

WALIMU WAJANJA MKOANI PWANI STOP KUCHANGISHA MICHANGO KWA WANAFUNZI/WAZAZI


Kaimu katibu tawala mkoani Pwani,Edward Mwakipesile,akizungumza jambo,na baadhi ya wadau wa elimu na watendaji mkoani humo juu ya masuala mbalimbali ya kielimu.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
KAIMU katibu tawala mkoani Pwani,Edward Mwakipesile,amewaasa baadhi ya walimu wajanja wa shule msingi na sekondari ,mkoani hapo,kuacha kuchangisha michango kinyemela kwa wanafunzi ama wazazi.
Aidha amewataka wazazi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ,wahakikishe watoto hao wanaripoti kwenye shule walizopangiwa pasipo kuwaacha majumbani.
Katika upande mwingine ,Mwakipesile ametoa rai kwa jamii kuwaandikisha watoto wao wenye umri wa kuanza shule ya msingi kwani elimu ni silaha ya kupambana na adui ujinga.
Akizungumza na wadau wa elimu na baadhi ya watendaji mkoani humo,katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Pwani,alisema hataki kusikia kuna mwalimu anachangisha mzazi mchango wa aina yoyote.
Alieleza kuwa serikali ilitangaza elimu bila malipo kwa wanafunzi wa awali,msingi hadi kidato cha nne,na wizara ya elimu ilitoa waraka wa elimu kuhusu elimu bila malipo kwa kila mwanafunzi.
Mwakipesile alisema kwamba ,walimu wanatakiwa kusimamia utekelezaji wa sera hiyo ili wasitokee walimu wachache watakao haribu mpango huo.
Hata hivyo alisema kwa upande wa mzazi na mlezi pia hakuna haja ya kisingizio cha kushindwa kuwasomesha watoto wao .
Mwakipesile alifafanua ,ni marufuku mwalimu yeyote kuchangisha michango mbalimbali kinyemela na atakaebainika kufanya hivyo atawajibishwa.
Alisema hakuna mwalimu mwenye mamlaka ya kuchangisha michango mashuleni bali mwenye mamlaka ya kuruhusu kuchangisha ni mkuu wa mkoa tena akiona inafaa kufanya hivyo na sio vinginevyo.
Mwakipesile akizungumzia kuhusu suala la kupeleka watoto shule ,alisema ujanja wa sasa ni elimu na ni ufunguo wa maisha .
“Katika maeneo yetu haya baadhi ya watu bado hawajagundua umuhimu wa elimu,kuanzia sasa mkakati tuliojiwekea ni sekretariet ya mkoa itafuatilia hadi kwenye shule binafsi na shule za serikali”
“Wapo wazazi wanaodanganya kuwa watoto wao wapo katika shule binafsi kumbe wanaongopa na kukuta kumbe mtoto yupo nyumbani hajapelekwa shule kwa makusudi”alisema Mwakipesile.

Alibainisha, mkoa huo umekamilisha zoezi la upatikanaji wa madawati na hakuna mtoto anaekaa chini ambapo sasa inajikita kujenga na kuboresha miundombinu ikiwemo madarasa.

Mwakipesile alisisitiza, nguvu ielekezwe kwenye miundombinu na kuboresha mazingira mazuri kwa wanafunzi ili kuinua taaluma zao.
Nae kaimu afisa elimu mkoani hapo,Modest Tarimo,alisema wanafunzi 15,528,wamefaulu kwenda kujiunga na elimu ya sekondari  mwaka 2017 baada ya kufanya mtihani wa darasa la saba.

Alisema changamoto kubwa inayowakabili kwenye sekta ya  elimu ni utoro kwa wanafunzi na baadhi ya wazazi  kukosa mwamko wa elimu.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania