CURRENT NEWS

Thursday, January 19, 2017

DC MTATURU ATAKA MKANDARASI ARRAY KUTOPEWA TENDA ZA HALMASHAURI YA IKUNGI              


Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akikagua ujenzi wa daraja kubwa la Minyughe linalojengwa kwa thamani ya shilingi milioni 924.6 na kutajwa kuwa kiungo muhimu kwa wananchi wa kata za Sepuka,Irisya,Makilawa,Minyughe,Puma na Ihanja baada ya kukamilika kwake.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu akipoke taarifa ya ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule ya sekondari Wembere.
Mafundi wa kutoka kampuni ya ujenzi ya Kings Builders& General Services LTD wakiendelea na ujenzi wa daraja kubwa la Minyughe lililopo wilayani Ikungi linalotarajiwa   
Kukabidhiwa machi mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu akiwa ameambatana Kaimu Afisa Mtendaji wa kata ya Wembere katika ukaguzi wa ujenzi wa matundu ya choo kwenye shule ya sekondari Wembere.
                   ..........................................................................................................
KATIKA moja ya mikakati ya serikali ya awamu ya tano chini ya rais dokta John Magufuli ni kuhakikisha kunakuwepo mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ambapo katika kusimamia hilo mkuu wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu amefanya ziara ya kukagua miradi iliyopo katika mpango wa serikali wa kuwezesha shule za sekondari nchini(SEDEP).

Katika ziara hiyo Mtaturu amekagua ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo katika shule ya sekondari ya Minyughe,Wembere na Msungua na kutoa agizo kwa mkurugenzi la kuvunja mkataba wa mkandarasi ARRAY TECH SERVICES LTD.

Aidha amepiga marufuku mkandarasi huyo kupewa kazi tena katika wilaya hiyo.

Hatua hiyo inatokana na mkandarasi huyo kwenda kinyume na mkataba ikiwemo kujenga chini ya kiwango.

“Mkandarasi huyu alipewa kazi ya kujenga madarasa mawili katika sekondari ya Iseke na matundu ya vyoo 10 katika shule ya Minyughe lakini ameenda kinyume cha mkataba.,”alisema Mtaturu.

Kutokana na hilo amewasisitiza watendaji kuepuka kutoa tenda  kwa mkandarasi yoyote bila ya kujua historia yao ya kazi.

Ujenzi mwingine uliopo ni wa nyumba za walimu katika shule ya sekondari ya Minyughe  na Wembere ambapo kukamilika kwake zitasaidia kupunguza tatizo la makazi kwa  walimu na hivyo kuongeza ari ya ufundishaji na  kuongeza kiwango cha   ufaulu.

Mbali na kukagua ujenzi wa madarasa pia Mtaturu amekagua ujenzi wa daraja kubwa la Minyughe linalojengwa na mkandarasi KINGS BUILDERS AND GENERAL SERVISEC LTD kwa thamani ya shilingi milioni 924.6 linalotarajiwa kukabidhiwa mwenzi machi mwaka huu.

Kukamilika kwa daraja hilo kutakuwa kiungo muhimu kwa wananchi wa kata za Sepuka,Irisya,Makilawa,Minyughe,Puma na ihanja.

Mtaturu amesema kwa sasa wananchi wanazunguka umbali wa kilomita 80 kwenda makao makuu ya wilaya lakini kukamilika kwa daraja hilo kutawafanya wananchi hao kutumia chini ya kilomita 40 hatua ambayo itaongezea uchumi kwa wakulima na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi kama ilivyoanishwa katika Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania