CURRENT NEWS

Saturday, January 14, 2017

DIWANI BWARWANI AINGILIA KATI MGOGORO WA ARDHI KATIKA KIJIJI CHA VIGWAZA


 Diwani wa kata ya Vigwaza,Mohsin Bwarwani ,akizungumza na wakazi wa kijiji cha Vigwaza ili kuweka suluhu ya mgogoro wa ardhi.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Vigwaza
DIWANI wa kata ya Vigwaza,wilaya ya Bagamoyo,Mohsin Bwarwani ameingilia kati mgogoro wa ardhi ya hekari 80 ,uliokuwa ukifuka miaka mingi ,kijiji cha Vigwaza na kuupatia ufumbuzi .
Diwani huyo aliitisha mkutano wa wananchi ili kutoa ufafanuzi juu ya mgogoro huo ambapo kwa pamoja waliridhia hekari 59 kuachiwa mwekezaji James Kombe na hekari 21 kubakia kwa matumizi ya maendeleo ya kijiji.
Bwarwani alieleza kuwa mgogoro huo ni wa muda mrefu uliokuwa ukihitaji ufafanuzi kutoka kwa viongozi waliopita na si vinginevyo.
Aidha aliwaagiza watendaji wa kijiji cha Vigwaza na Kitonga ambae zamani alikuwa mtendaji wa kijiji cha Vigwaza kuangalia muhtasari wa maamuzi ya  mkutano mkuu uliokaa wakati wa uongozi uliopita ili usomwe kwenye mkutano mkuu wa kijiji ujao.
Alisema muhtasari huo utasaidia kuonyesha kumbukumbu ya makubaliano yaliyoridhiwa wakati huo na kuondoa mashaka kwa wananchi.
“Mali bila daftari hupotea bila habari,nashukuru wakati nikiwa mwenyekiti wa kijiji hiki kabla sijawa diwani tulikuwa tukiweka kumbukumbu,itasaidia kuonyesha yaliyojiri “alisema Bwarwani.
Bwarwani alisema wakati anakabidhi majukumu kwa uongozi mpya walikabidhi nyaraka na maelezo kamili juu ya eneo hilo .
Hata hivyo alieleza ,sakata hilo lipo wazi limalizwe na wananchi wafanye shughuli nyingine za kujiendeleza kimaisha .
Bwarwani aliwataka wakazi wa Vigwaza kujenga tabia ya kuamini viongozi wao kwa yale wanayoyatekeleza kuwatumikia wananchi badala ya kuweka dhana ya kuwepo kwa ubadhilifu kwenye kila jambo.
Alisema ni wakati wa wananchi kumtumia mwekezaji huyo kwa kushirikiana nae katika shughuli za kijamii.
Mwenyekiti wa kijiji cha Vigwaza ,Ramadhani Kirumbi,alisema katika mkutano wa kijiji waliouitisha jan 3 mwaka huu,wananchi waliazimia serikali ya kijiji hicho uwasiliane na mkuu wa mkoa wa Pwani  ili aingilie kati mgogoro huo.
Alisema anashukuru kabla ya kuchukua hatua diwani wa kata hiyo ametumia busara na kwenda kumaliza mgogoro ambao uliihitaji ufafanuzi kutoka kwa viongozi waliopita.
Kirumbi alieleza kwamba wameridhia kati ya hekari 80,sasa hekari 59 zitakuwa za mwekezaji James Kombe na nyingine 21 zimerudi rasmi kwa kijiji.
Alifafanua kuwa kutokana kwasasa mwekezaji huyo atatakiwa kulipia kiasi cha sh.mil 5.2 kama asilimia ya kijiji kulingana na ardhi aliyoinunua.
Kwa upande wake, Mariamu Swala na Sheikhdeli Mikole walisema ifike tamani mwa tatizo hilo ili watu wafanye mambo mengine ya maendeleo.
Sheikhdeli alisema masuala hayo yapo wazi kwani halmashauri ya kjiji iliyopita ilikuwa ikikaa vikao na kushirikisha kamati ya ardhi ambayo iliingilia mgogoro huo na mkutano mkuu uliitishwa na wananchi waliridhia.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania