CURRENT NEWS

Wednesday, January 11, 2017

JAFO AAGIZA MA-DC KUWACHUKULIA HATUA WAZAZI WASIOPELEKA WATOTO SHULE

 Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Seleman Jafo akizungumza baada ya kuridhishwa na utendaji wa kazi ya ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Chang’ombe ‘A’ na ukarabati wa majengo ya shule wakati wa ziara aliyoifanya katika shule hiyo leo.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo akitoka kukagua ujenzi wa choo cha walimu katika shule ya msingi Chang’ombe ‘B’ wakati wa ziara yake aliyoifanya katika kata ya Chang’ombe.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)  Seleman Jafo akiwa na mwanafunzi George John wa darasa la saba ambaye ni mlemavu  na kutoa agizo kwa  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma  Godwin Kunambi,kuhakikisha mradi wa ujenzi wa vyoo vya wanafunzi Shule ya Msingi Chang’ombe 'A' unazingatia miundombinu rafiki kwa ajili ya watu wa ulemavu wakati wa ziara yake aliyoifanya katika kata ya Chang’ombe.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo akipokea maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma  Godwin  Kunambi juu ya ukamilifu wa ujenzi wa choo cha walimu shule ya msingi Chang’ombe ‘B’ pia uendelevu wa ujenzi wa vyoo vya wanafunzi  katika ziara yake aliyoifanya katika kata ya Chang’ombe.

     .....................................................................................................

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo amewaagiza Wakuu wa wilaya nchini kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wanakwenda kuanza shule huku akiwasisitiza wazazi watakaoshindwa kuwapeleka shule watoto hao wachukuliwe hatua za kisheria.

Jafo ametoa agizo hilo leo alipofanya ziara ya kukagua miundombinu mbalimbali katika shule za msingi, Chadulu, Chang’ombe A na B, Manispaa ya Dodoma.

Katika ziara yake ya kukagua maagizo aliyoyatoa kwenye shule hizo kuhusu masuala ya miundombinu, Jafo amesema  “Sisi kama serikali hatutaki mtoto akose elimu hasa katika kipindi hichi ambacho serikali imeamua kuelekeza nguvu za kutosha kwenye elimu kwa ajili ya watanzania.”

Ameongeza “Kwa mzazi ambaye mtoto wake atabainika hajaenda shule na kupewa kazi zingine kama kuendesha bodaboda hatua za kisheria zichukuliwe mara moja,”.

 Pamoja na hayo, Jafo amekemea tabia ya wazazi kutotilia mkazo masuala ya elimu na kuwakabidhi watoto wao kuendesha bodaboda kama ajira yao badala ya kuwapeleka shule na kuwataka kuhakikisha wanawanunulia mahitaji yote ya shule.

Aidha amesema serikali haitarajii kuna vijana waliochaguliwa wakishawishiwa na wazazi kufanya vibaya kwenye mitihani kutokana na elimu kuwa ni bure.

Akizungumzia kuhusu watoto walioandikishwa kuanza kusoma elimu ya awali na msingi, Jafo amesema kumekuwepo na mwitikio mkubwa katika suala la uandikishaji watoto hao na linatokana na uwepo wa elimu bure.

Hata hivyo, amesema shule nyingi idadi ya wanafunzi imeongezeka zaidi na kwa serikali ni faraja kuona watanzania wengi sasa wanapata elimu huku akiwataka wazazi wahakikishe watoto walioandikishwa wanahudhuria shule ipasavyo  na wakurugenzi kuendelea kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Kadhalika, Jafo ameridhishwa na ukarabati wa miundombinu mbalimbali kwenye shule hizo huku akiwaahidi walimu kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, amesema kwasasa Manispaa hiyo inaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja ujenzi wa shule za msingi na sekondari na kuongeza madarasa kwenye baadhi ya shule ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi hasa wanaohamia Dodoma.

 Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Manispaa hiyo, Scholastika Kapinga, amesema hadi sasa watoto zaidi ya 8,000 wameandikishwa kwenye manispaa hiyo kuanza kusoma elimu ya awali na msingi.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania