CURRENT NEWS

Saturday, January 7, 2017

JAFO-FEDHA ZA BASKET FUND ZISIGEUZWE KICHAKA CHA ULAJI NA KUVIMBISHA MATUMBO

 Naibu waziri ofisi ya rais na serikali za mitaa TAMISEMI,Selemani Jafo akizungumza jambo na watumishi wa kituo cha afya Mlandizi katika ziara yake ya kawaida mkoani Pwani akiwa Kibaha.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Kaimu mganga mfawidhi kituo cha afya Mlandizi,Dkt Herzon Mwakibughi akitoa taarifa ya kituo hicho kwa naibu waziri ofisi ya rais na serikali za mitaa TAMISEMI,Selemani Jafo alipotembelea kituoni hapo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

NAIBU waziri ofisi ya rais na serikali za mitaa (TAMISEMI)Seleman Jafo,amekemea tabia ya baadhi ya wakuu wa idara ya afya na halmashauri nchini kugeuza fedha za mfuko wa wahisani katika kuboresha huduma za afya(basket fund) kuwa kichaka cha ulaji na kusababisha kudidimiza huduma za kiafya.

Aidha amemuagiza mganga mkuu wa wilaya ya Kibaha(DMO) kusimamia na kupitia muongozo wa fedha za mfuko huo ambazo zimeshapelekwa katika halmashauri zote mbili wilayani hapo ili kuhakikisha zinatumika ipasavyo.

Sambamba na hayo Jafo amemtaka mganga mkuu huyo na mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi kusimamia kituo  hicho maana inaonekana kuna jambo sio shwari .

Akizungumza na watumishi wa kituo cha afya mlandizi,wakati wa ziara yake ya kawaida mjini Kibaha,alisema ulaji wa fedha hizo unahusisha mtandao wa baadhi ya waganga wakuu wa wilaya,mikoa,wakurugenzi na waweka hazina .

Jafo alisema mchezo huo uachwe mara moja na badala yake fedha hizo zitumike kikamilifu kutatua changamoto za kiafya ikiwemo madawa na vifaa tiba.

“Kuna mtandao huo unaumiza wananchi wenye mahitaji ya huduma bora za kiafya pamoja na 
watalaamu wa afya waliopo chini kupata shida”alisema Jafo.


Jafo alieleza kwamba kuna changamoto ya matumizi ya mfuko wa basket fund katika halmashauri nyingi hapa nchini na badala yake kuzitumia katika matumizi mengine yasiyo lengwa .

Halmashauri ya wilaya ya Kibaha wametumia kiasi cha sh mil.17 kununua dawa kati ya sh.mil 90 walizopokea katika mfuko huo wakati zilitakiwa wanunue dawa za mil.30 kulingana na muongozo wa kutumia asilimia 33 ya fedha inayopokelewa.


Jafo alifafanua kuwa katika wilaya ya Mkuranga walitakiwa wanunue dawa za mil.86 lakini wamenunua chini ya sh mil.20 jambo ambalo ni kinyume na taratibu zilizopo.

Alisema ugonjwa huo wa kutofikia malengo ya matumizi ya mfuko huo upo kila wilaya na kila mwaka wakidai kuna upungufu wa dawa wakati fedha za kununulia madawa zipo.

Jafo alibainisha,maeneo mengi fedha hizo hazitumiki sawa sawa zimekuwa kama kichaka cha kula fedha na mwaka ukiisha fedha hizo zinarudishwa serikalini kwasababu mfuko huo una muongozo wa matumizi yake.


“Nakuagiza DMO kusimama sawa sawa,nitakuwa nikipita mara kwa mara ,hakuna excuse kwa hili tena,simamia miongozo na utaratibu wote.’hawa madiwani wanapata tabu kupigiwa kelele na wananchi kuhusu kero ya ukosefu wa dawa kila kukicha”.


“Juzi nilisoma gazeti moja la hapa nchini ,mbunge wa jimbo hili Hamoud Jumaa akilalamika kuwa hali ya kituo cha afya Mlandizi sio shwari, lisemwalo lipo,inaonyesha hakuna uongo juu ya hili,inaonekana management haipo sawa maana kuna makambale wakubwa na wadogo fanyeni kazi kwa bidii”

Jafo aliwataka mganga mkuu wa wilaya na mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi kusimamia kituo  hicho maana inaonekana kuna jambo sio shwari .

Aliwataka watumishi,wauguzi na waganga kituoni humo kuhudumia wananchi kwa kufuata maadili yao ya kazi ili kuimarisha huduma ya afya.


Kaimu mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi,Herzon Mwakibughi ,alitaja changamoto zinazowakabili ni uhaba wa madawa,vitanda vya kulazia wagonjwa na ukosefu wa mashine ya kufulia suala linalosababisha kwenda kufulia hospitali ya rufaa ya Tumbi.


Alitaja changamoto nyingine ni ukosefu wa X-ray na kupelekea usumbufu kwa wagonjwa hasa majeruhi wa ajali,jokofu la kuhifadhia maiti na ukosefu wa uzio hali inayosababisha wananachi kuleta usumbufu kwa wagonjwa.

Kaimu mkuu wa wilaya ya Kibaha,Happiness Seneda aliomba ofisi za mkurugenzi,mkuu wa wilaya,mkoa,wakuu wa idara ,mabaraza ya madiwani na watumishi kujenga ushirikiano.

Happiness alisema umoja na ushirikiano katika maeneo ya kazi ni nguzo pekee itakayowezesha kupiga hatua kimaendeleo na kiuchumi kwa haraka.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania