CURRENT NEWS

Thursday, January 19, 2017

JESHI LA POLISI PWANI LAKAMATA WAHAMIAJI HARAMU 361 NDANI YA MWAKA MMOJA ULIOPITA


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
JESHI la polisi mkoani Pwani, limewakamata wahamiaji haramu 361 kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Ethiopia ,katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Januari hadi desemba 2016.
Aidha gari moja lililotumika kusafirisha wahamiaji haramu lilitaifishwa na dereva wake kufungwa kifungo cha miaka 20 jela.
Hayo yaliwekwa wazi na kamanda wa polisi mkoa wa Pwani,Boniventure Mushongi,wakati akitoa tathmini ya matukio yaliyotokea mwaka uliopita mkoani humo na namna ilivyojipanga kudhibiti njia za panya za kuingia wahamiaji haramu .


Alisema kuwa watuhumiwa wote hao walifikishwa mahakamani kwa kushirikiana na idara ya Uhamiaji.
Mushongi alieleza kwamba nchi ya Ethiopia ndiyo iliyokuwa na idadi kubwa ya wahamiaji haramu ambao ni 343 ikifuatiwa na Burundi wahamiaji haramu tisa, Kongo watatu na Kambodia, Zambia, Afrika ya Kusini, Kameruuni na Malawi ambazo zilikuwa na wahamiaji haramu mmoja kila nchi. 
Alisema katika kukabiliana na uhalifu huo serikali ilitunga sheria kazi ambapo kwa sasa wasafirishaji wanapokutwa na hatia hufungwa jela miaka 20 ama faini ya sh.mil 20 na gari husika kutaifishwa.
Mushongi alibainisha kuwa moja ya watu waliokutwa na hatia ni dereva wa gari namba T 786 BBX aina ya Mitsubishi Canter ambaye alihukumiwa kwenda jela miaka 20 kwa kosa la kukutwa na hatia ya kusafirisha wahamiaji haramu .


“Moja ya sababu zinazosababisha kukamatwa wahamiaji haramu ni kutokana na mkoa huo kuwa mapitio yao kuelekea Jijini Dar es Salaam na kuendelea na safari zao hasa Kusini mwa Afrika”alisema Mushongi.
Hata hivyo alisema wahamiaji haramu wamekuwa wakiwakamata mara kwa mara kutokana kupata taarifa kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakionyesha ushirikiano na jeshi la polisi.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania