CURRENT NEWS

Friday, January 27, 2017

JUMAA AANZA UJENZI WA UZIO KATIKA KITUO CHA AFYA MLANDIZI UTAKAOGHARIMU MIL. 200

 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa akichimba udongo kwenye eneo zilipowekwa alama za ujenzi wa uzio katika kituo cha afya Mlandizi, ambao utagharimu mil. 200 hadi kukamilika kwake. (picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwisho, Kibaha
Mbunge wa jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa ameanza mchakato wa ujenzi wa uzio wa kituo cha afya Mlandizi,utakaogharimu sh.mil 200,hadi kukamilika kwake.
Kuanza kwa ujenzi huo kunaleta matarajio ya kuondoa kilio cha miaka mingi cha ukosefu wa uzio kituoni hapo.
Akizungumzia wakati wa kupima na kuweka alama za ujenzi wa msingi wa ukuta huo, Jumaa alisema hiyo ni moja ya ahadi zake alizotoa hivi karibuni.
Alielezea kuwa ukosefu wa uzio katika kituo cha afya mlandizi kunasababisha watu kupita ndani ya kituo na kupelekea usumbufu kwa wagonjwa.
Jumaa alisema, kwa sasa amejipanga kwenda sambamba na kauli mbiu yake ya "Sisi kwanza serikali baadae ".
"Tunahitaji kituo hiki kipandishwe hadhi na kuwa hospital ya wilaya hivyo hatuna budi kutekeleza vigezo vinavyotakiwa ili tufikie malengo hayo"
"Niwaombe tuu wadau wa afya na serikali kuniunga mkono kwa hili hatimae tuondoe tatizo hili la ukosefu wa ukuta "alisema Jumaa.
Nae mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mlandizi,dk.Mpola Tamambele,alisema kuanza kwa hatua za awali za ujenzi huo kunawapa faraja.
Alibainisha kwamba, awali makamu wa rais nchini aliahidi kuwajengea uzio huo lakini bado walikuwa wakisubiria utekelezaji.
Dk.Tamambele alisema, mwishoni mwa mwaka jana, mbunge huyo alikwenda kuwatembelea na walimweleza kero zao ambapo aliahidi kuzitatua kwa awamu kulingana na uwezo wake.
Alitaja changamoto ambazo zinazowakabili ni uhaba wa madawa,vitanda vya kulazia wagonjwa na ukosefu wa mashine ya kufulia suala linalosababisha kwenda kufulia hospitali ya rufaa ya Tumbi.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa X-ray na kupelekea usumbufu kwa wagonjwa hasa majeruhi wa ajali na,jokofu la kuhifadhia maiti .
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania