CURRENT NEWS

Tuesday, January 24, 2017

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA MKURUGENZI MKUU WA UNEP

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na  Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Bw. Erik Solheim ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku 2.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na  Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Bw. Erik Solheim ambaye ameongozana na ujumbe wake kwa ziara ya siku 2 wengine waliohudhuria ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba (kulia) na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Faustine Kamuzora.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba akifafanua jambo wakati wa mkutano wa  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  na  Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Bw. Erik Solheim na ujumbe wake .

                             ............................................................................
 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameliomba Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kuisaidia Tanzania kukabiliana na tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira katika maeneo mbalimbali nchini ambao umepelekea mamia ya ekari za misitu kutoweka kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema pamoja na Serikali kufanya jitihada kubwa za kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira ikiwemo mpango wa upandaji wa miti kote nchini lakini bado msaada na nguvu zaidi inahitajika kutoka shirika la Mazingira la UNEP ili kuongeza kasi ya kukabiliana na tatizo hilo nchini.
Amesema Tanzania ina mahusiano mazuri na ya muda mrefu na Shirika la UNEP ambapo shirika hilo limeweza kuisaidia nchi katika miradi mbalimbali ya kuhifadhi mazingira hivyo mahusiano hayo mazuri ni muhimu yakaja na mbinu bora na nzuri za kuhifadhi mazingira ili kuokoa Taifa lisigeuke jangwa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea nchini.

Makamu wa Rais pia amehimiza wataalamu wa mazingira wajikite zaidi katika kutoa elimu kwa wananchi watumie nishati mbadala kama gesi na makaa ya mawe ili kudhibiti tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ERIC SOLHEIM amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira na kusisitiza kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali Tanzania katika Uhifadhi wa mazingira nchini.


Mkurugenzi huyo amesema suala la kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira sio la Serikali pekee hivyo ni muhimu kwa Serikali kushirikiana ipasavyo na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kupambana na tatizo ili kupata suluhu ya kudumu.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira January Makamba amesema ujio wa Mkurugenzi Mkuu wa UNEP hapa nchini ni fursa ya kipekee ya kufungua na kuimarisha ukurasa mpya wa mahusiano kati ya Tanzania na UNEP.
Makamba amesema kuwa Serikali imetengeneza programu mpya Tano za mazingira ikiwemo kupunguza matumizi ya mkaa ili kuhifadhi misitu,vyanzo vya maji,kushughulikia taka na kujenga uwezo kama hatua mpya kabisa ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania