CURRENT NEWS

Tuesday, January 17, 2017

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA KINGDOM LEADERSHIP NETWORKS

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania Ibrahimu Kaduma aliyemtembelea Makamu wa Rais na kumuelezea mikakati ya kuanzisha Chuo cha Joseph Business School.
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania Ibrahimu Kaduma aliyemtembelea Makamu wa Rais na kumuelezea mikakati ya kuanzisha Chuo cha Joseph Business School kushoto ni Meneja Mradi Dkt Charles Sokile.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania uliomtembelea ofisini kwake, Ikulu jijini Dar es Salaam.
                                   ..............................................................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameuhimiza uongozi wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania kuharakisha mchakato wa kuanzisha Chuo cha Joseph Business School hapa nchini chuo ambacho kitatoa mafunzo mbalimbali ya biashara, maadili ya uongozi na ugunduzi wa mawazo ya biashara ili kusaidia mamia ya Watanzania kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Makamu wa Rais ametoa kauli ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa  Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania ambao walimtembelea Makamu wa Rais kumweleza hatua ambazo wamefikia katika uanzishaji wa Chuo hicho.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema wazo la uanzishaji wa Chuo hicho ulitolewa na Dkt Bill Winston ambaye ni Mwanzilishi wa Winston Ministries mwaka jana katika Maombezi ya Taifa ambaye yeye alikuwa mgeni rasmi katika maombi hayo, anasema aliupokea kwa furaha mpango huo kwa sababu chuo hicho kitasaidia watanzania wengi kupata elimu na ujuzi wa kuimarisha biashara zao wakati taifa likielekea kwenye uchumi wa Viwanda.

Amesema hatua za uanzishwaji wa Chuo hicho hapa nchini ni fursa pekee na nzuri kwa Watanzania kujifunza ubunifu na ugunduzi katika biashara, maadili ya uongozi katika biashara ili kuongeza ufanisi katika biashara zao kwa ajili ya manufaa yao na taifa kwa ujumla hasa katika ulipaji wa kodi.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania Ibrahimu Kaduma na Meneja Mradi Dkt Charles Sokile wamemhakikishia Makamu wa Rais kuwa hatua ambazo wamefikia kwa sasa katika uanzishaji wa Chuo hicho ni nzuri ambapo mpaka sasa wamepata majengo kwa ajili ya ofisi na maeneo ya kufundishia na hatua za usajili wa chuo hicho zipo katika hatua za mwisho.

Wamesisitiza kuwa wanataka kushirikiana ipasavyo na Serikali katika uanzishaji wa chuo hicho ambacho kitatoa elimu ya biashara hasa ugunduzi wa mawazo ya biashara nchini kama hatua ya kutekeleza kwa vitendo dhana ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda nchini.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania