CURRENT NEWS

Monday, January 16, 2017

MAKOSA MAKUBWA IKIWEMO UNYANG'ANYI WA KUTUMIA NGUVU/SILAHA NA MAUAJI YAONGEZEKA PWANI


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKOA wa Pwani,umekuwa na ongezeko la makosa makubwa 4,208 yaliyoripotiwa katika mwaka 2016 ambapo makosa ya yaliyochukua nafasi kubwa ni unyang’anyi wa kutumia nguvu,kupatikana silaha na mauaji.
Ongezeko hilo ni la makosa 419 ukilinganisha na makosa yaliyoripotiwa mwaka 2015 yaliyokuwa 3,784 .
Aidha makosa madogo 16,332 yaliripotiwa katika kipindi hicho cha mwaka 2016 ambapo kuna ongezeko la makosa 2,396 ikilinganishwa na mwaka 2015 uliokuwa na makosa 13,936.
Akitoa taarifa ya mwaka uliopita kwa waandishi wa habari,ofisini kwake,kamanda wa polisi mkoani Pwani Boniventure Mushongi ,alisema ,hali hiyo inawapa nguvu ya kuongeza kasi ya kupambana/kudhibiti njia za panya na njama wanazotumia wahalifu.
Hata hivyo alieleza,katika kipindi cha Jan hadi desemba 2016 ,kumekuwepo na baadhi ya matukio yaliyovuta hisia za watu ikiwemo tukio kupatikana kwa miili ya watu saba kwa nyakati tofauti wilayani Bagamoyo.
Alitaja matukio mengine ni yaliyosababisha vifo vya viongozi wa serikali za za vijiji kwa Mkuranga ,Rufiji na Kibiti ambapo watu 11 walikamatwa na wameshafikishwa mahakamani.
Mushongi alisema kati ya makosa yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi ni pamoja na unyang’anyi wa kutumia nguvu makosa 294 ukilinganisha na makosa 197 yaliyoripotiwa 2015 hivyo kuwa na ongezekjo la makosa 57.
Makosa mengine ni kupatikana kwa silaha makosa 25 ambapo 2015 yalikuwa 20 ongezeko 5 na makosa ya mauaji kwa mwaka 2016 ni 126 huku 2015 yakiwa 107 tofauti 19.
Makosa mengine ni unyang’anyi wa kutumia silaha ,uvunjaji,magendo makosa 52,na makosa ya kubaka yameongezeka kutoka 340 hadi kufikia 416 mwaka 2016.
Mushongi alieleza kuwa,ongezeko la makosa hayo imetokana na misako iliyofanywa, doria na oparesheni zilizokuwa zikifanywa kwenye maeneo mbalimbali na kushirikisha jamii.
“Tunawashukuru wananchi ,wasamaria wema,kwa ushirikainao wao na jeshi letu,tunawaomba waendelee na ushirikiano huo wa kutoa taarifa mbalimbali ambazo zinasaidia kukabiliana na uhalifu “
“Uwiano wa askari na raia bado hautoshi kwani askari mmoja anahudumia raia zaidi 1,000 hivyo ulinzi shirikishi ni muhimu ndani ya jamii,” alisema Mushongi.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita walifikisha mahakamani makosa 1,439 sambamba na hilo watuhumiwa wa makosa 159 walikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo wakati makosa 29 watuhumiwa walishindwa kutiwa hatiani na kuachiwa huru.
Jeshi hilo licha ya kukabiliana na wahalifu mbalimbali lakini linakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na uchache wa magari,Jiografia ya mkoa kwenye mipango miji ni ngumu kumpata mhalifu kwa haraka pindi uhalifu unapotokea.
Muingiliano na mkoa wa Dar es Salaam unafanya wahalifu kuweza kuingia kirahisi na kufanya makosa na uuwepo wa ukanda wa mkubwa katika bahari unaosababisha kuwepo kwa bandari bubu nyingi za kupitisha wahamiaji haramu na biashara za magendo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania