CURRENT NEWS

Wednesday, January 25, 2017

MBUNGE HAMOUD JUMAA ALILIA WILAYA YA KIPOLISI MLANDIZI

MBUNGE wa Kibaha Vijijini,Hamoud Jumaa,akizungumza wakati alipokwenda kutembelea kituo cha polisi Mlandizi,kujionea ujenzi wa makazi ya polisi,kulia ni mkuu wa kituo hicho,mrakibu Silvester Njau.
Mkuu wa kituo cha polisi Mlandizi,mrakibu Silveter Njau akionekana kuchanganya udongo kwenye ujenzi wa makazi ya polisi yanayojengwa karibu na kituo hicho.
 Mbunge wa Kibaha Vijijini,Hamoud Jumaa,akichanganya udongo kwenye ujenzi wa makazi ya polisi yanayojengwa karibu na kituo cha polisi Mlandizi.(Picha na Mwamvua Mwinyi.)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini,mkoani Pwani, Hamoud Jumaa,ameiomba wizara ya mambo ya ndani ,kubariki ombi la kituo cha polisi Mlandizi kuwa wilaya ya kipolisi.
Mbali ya hilo amesema endapo kituo hicho,kitapatiwa gari jipya itasaidia kuwa na usafiri wa uhakika ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Aidha Jumaa ,ameahidi kuchangia kiasi cha sh.mil.tano kwenye ujenzi wa nyumba za polisi zinazoendelea kujengwa karibu na kituo hicho.
Hayo aliyasema wakati akizungumza na askari polisi wa kituoni hapo kisha kwenda kujionea hatua za ujenzi wa nyumba hizo ulipofikia.
Mbunge huyo alisema awali alishatoa mil.moja kwa ajili ya kununulia mchanga wakati ujenzi ulipoanza na pikipiki mbili.
Askari hawa wanakabiliwa na changamoto ya kuishi uraiani kwenye nyumba za kupanga kutokana na ukosefu wa makazi kwa ajili yao ,ukosefu wa nyumba za polisi kunasababisha kuchelewa kutekeleza kazi zao”alisema Jumaa.
Jumaa alisema mkuu wa kituo hicho,mrakibu Silvester Njau aliona mbele na kuanzisha ujenzi huo ili kuwakomboa baadhi ya polisi.
Alieleza kwamba,kutokana na juhudi hizo yeye akiwa ni mbunge wa jimbo hilo,ameamua kuunga mkono suala hilo.
Akizungumzia kituo cha polisi Mlandizi kuwa wilaya ya kipolisi,alisema wizara husika inapaswa ilione hilo kwani kituo hicho ni kikubwa na mji unazidi kukua siku hadi siku.

Jumaa alifafanua kuwa ,kikipanda hadhi kitakuwa na uwezo mkubwa na hatua hiyo itawezesha kupata mahitaji ya usafiri na vitendea kazi kirahisi.

Mkuu wa kituo cha polisi Mlandizi,mrakibu Silvester Njau alieleza tatizo la ukosefu wa makazi ni kubwa ndipo alipoamua kuanzisha ujenzi ambapo utakapokamilika utawezesha kuishi familia tatu hadi sita .
“Kwasasa askari wote tunaishi uraia ambako ni mbali ikiwemo Chalinze,Kibaha,Mbezi,Kiluvya ,Kibamba hivyo kutuweka katika wakati mgumu na mazingira ya kazi”
“Ukimwita askari may be usiku inakuwa ni ngumu sana kufika ukizingatia usafiri wa public nyakati za usiku mwingi unakua haupo hivyo ni changamoto kubwa”alisema mrakibu Njau.
Mrakibu Njau ,alisema kila mmoja anajukumu la kulinda nchi hivyo anaomba wadau wa amani ajitokeze kuchangia kwa ari na mali ili kumaliza ujenzi huo.

Kituo hicho bado kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitendea kazi,usafiri na nyumba za polisi.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania