CURRENT NEWS

Thursday, January 5, 2017

MBUNGE JUMAA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KITUO CHA AFYA MLANDIZI NA KUVUMBUA MADUDU

 MBUNGE wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa ,mwenye kofia aina ya pama akionekana pichani akisaidiana na ndugu wa mgonjwa kumbeba kwenye kitanda kumpeleka wodini, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha afya cha Mlandizi.


 Mganga mfawidhi katika kituo cha afya  Mlandizi ,Dkt Mpola Tamambele ,akitoa magodoro na vitanda vya kupimia wagonjwa vya msaada kutoka kwa wadau mbalimbali,ambavyo walivifungia  pasipo kuvitumia ambapo mbunge wa Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaa alifanya ziara ya kushtukiza na kuamuru vitumike.


 Mbunge wa Kibaha Vijijini  Hamoud Jumaa akizungumza na baadhi ya watumishi ,wauguzi,madaktari katika kituo cha afya cha Mlandizi mara baada ya kutembelea wodi mbalimbali
Mbunge wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akiwakabidhi zawadi ya mabox ya vyombo vya jikoni  watumishi wote  katika kituo cha afya cha Mlandizi kama motisha na kuendelea kuwatia moyo kuwahudumia kiafya wananchi wa jimbo hilo .(Picha na  Mwamvua  Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha Vijijini
MBUNGE wa jimbo la Kibaha Vijijini ,Hamoud Jumaa,amefanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha afya Mlandizi na kuvumbua madudu ikiwemo baadhi ya wauguzi kwenye wodi ya uzazi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa.
Aidha katika ziara hiyo amekutana na malalamiko juu ya wauguzi wanafunzi wanaokwenda kufanya mafunzo kwa vitendo kituoni hapo,ambao wamekuwa wakitoa siri za maumbile ya akinamama wanaokwenda kujifungua nje ya kituo.

Kufuatia hali hiyo,Jumaa alimuasa mganga mfawidhi kituo cha afya Mlandizi na mganga mkuu halmashauri ya wilaya ya Kibaha,kuwachukulia hatua watumishi wazembe na wanatoa lugha chafu kwa wagonjwa .
Alisema amepokea pia  malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na wakunga na wauguzi katika wodi ya uzazi kutokuwa na lugha rafiki kwa akinamama wanaokwenda kujifungua.
Hata hivyo akiwa katika ziara hiyo alikuta vitanda vya wagonjwa katika wodi ya uzazi vikiwa havijatandikwa mashuka .
Mbali ya hilo mara baada ya kufika kituo cha afya Mlandizi,Jumaa alimkuta mama mmoja aliyejifungua watoto mapacha ambapo mtoto mmoja alifariki akiwa hana msaada wa kupelekwa wodini.
Mbunge huyo alimuuliza muuguzi aliyemkuta akibishana na ndugu wa mgonjwa na kisha kuamua kumbeba mama huyo pamoja na ndugu yake hadi wodini na aliendelea na matibabu.
Jumaa alisema baadhi ya wauguzi katika wodi hiyo na watumishi wamekuwa na dharau na maneno machafu kwa wagonjwa hali inayosababisha wananchi kukata tamaa yakufuata huduma kituoni hapo.
“Mimi mwenyewe nilikuja hapa saa 7 ya usiku na kwenda mapokezi ambako nilikutana na wadada wawili ,mmoja alinipokea vizuri lakini mwingine alinijibu maneno makali huku akiwa hajajua  mimi ni nani”
“Vitendo hivi havipendezi kwa wagonjwa hata kwa ndugu zao wanaowauguza ,kuweni wakarimu ,toeni huduma bora na upendo”alifafanua Jumaa.
Aliwaomba  watumishi na wahudumu hao kutimiza wajibu wao pasipo kuwanyanyasa akinamama hao kwani wanapofanya uzembe na manyanyaso ni chanzo cha vifo vya uzazi na watoto .

“Unakuta mtumishi ama mhudumu wa afya katika wodi ya uzazi anasuka ama wanapiga soga wakati kuna mama analalamika maumivu,wana wajibu maneno machafu, kiukweli watumishi wa aina hii lazima wawajibishwe”alisema Jumaa.Katika hatua nyingine alikuta vitanda vya kupimia wagonjwa na magodoro ambayo yalipelekewa kituoni hapo kama msaada kutoka kwa wadau mbalimbali vikiwa vimefungwa havitumiki.

Aliamuru magodoro hayo yawekwe katika baadhi ya vitanda kwenye wodi ya uzazi na vitanda vya kuhudumia wagonjwa wa kawaida vipelekwe kwa wagonjwa wa kawaida.

Hata hivyo alieleza kuwa ataendelea kutatua na kusimamia changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo katika sekta ya afya,maji,elimu na kusaidia makundi maalum ikiwemo vijana,walemavu ,wanawake na wazee.


Nae  kaimu mganga mkuu halmashauri ya wilaya ya Kibaha,Grace Boniface alisema amepokea malalamiko hayo na watasimamia maadili yanayotakiwa kitaaluma .
Alikemea tabia za kutoa siri za wagonjwa na kusema endapo watakwenda wanafunzi wauguzi kituoni hapo kuanzia sasa,' ni lazima kuwapa elimu na kuwarejesha katika maadili ya kazi hiyo ili kuepukana na matatizo hayo.

Grace alisema kila mtumishi atimize wajibu wake na ambae atashindwa basi atabeba mzigo wake mwenyewe kwani atalazimika kuondolewa kuondolewa kwenye nafasi yake.
Kwa upande wake mganga mfawishi wa kituo cha afya Mlandizi,Dkt Mpola Tamambele aliwataka watumishi kuendeleza umoja, upendo na mshikamano katika kuwapatia
huduma wagonjwa wanaofika kituoni hapo .

Alitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni sanjali na uhaba wa maji hasa wodi ya uzazi ,gloves ngumu katika wodi hiyo na ukosefu wa mashine ya kufulia hali inayosababisha  kufua kwa kutumia mikono.
Dkt Tamambele alitaja tatizo jingine ni uhaba wa madawa,vitanda vya kulazia wagonjwa ambavyo vingi ni vibovu na uhaba wa wodi ikiwemo ya akinamama na akina baba.
Ukosefu wa uzio hali inayopelekea watu kupita ndani ya kituo na kupelekea usumbufu kwa wagonjwa na kituo kudai kwamba kituo hicho ni kikubwa ,kinahudumia wagonjwa wengi hususan wa ajali za barabarani hivyo kinapaswa kupandishwa hadhi na kuwa hospitali ya wilaya.

Dkt Tamambele alisema awali kulikuwa na upungufu mkubwa wa vifaa tiba na mashine za kupimia magonjwa lakini kwa sasa kituo kinatoa huduma ya kupiga picha mionzi (utra sound) na kupima presha na kisukari.
Akijibu kuhusu kutotumia vitanda vya kupimia wagonjwa vilivyotolewa msaada na NMB alisema ,kweli wana upungufu wa vitanda hivyo lakini walifuata maelekezo kutoka juu.
Kituo cha afya Mlandizi kinahudumia zaidi ya wagonjwa 35,000 kwa mwezi kutoka wilaya ya Kibaha na maeneo jirani .
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania