CURRENT NEWS

Tuesday, January 24, 2017

DC IKUNGI AKUTANA NA MWAKILISHI WA WFP KUJADILI CHANGAMOTO ZINAZOKABILI MRADI WA CHAKULA SHULENI WILAYANI HUMO.


 Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akisalimiana na mwakilishi wa WFP kituo cha Dodoma Neema Nima Sitta baada ya kumaliza kikao cha makubaliano kuhusiana na mradi huo.
Kuanzia kushoto ni msimamizo wa shughuli za ugani kutoka WFP Ndg Saleh Mohamed, afisa elimu msingi Mwl Mohammed Bayu, mwakilishi wa WFP kituo cha Dodoma  Neema Nima Sitta, mkuu waw wilaya ya Ikungi Mhe Miraji J.Mtaturu, kaimu mkurugenzi wa  ndg halmashauri ya wilaya ya ikungi Haika Massawe, katibu tawala wa wilaya ya Ikungi  Winfrida Funto  na afisa kilimo Ndg Robert Chizinga wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza kikao cha makubaliano.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akiwa ofisini kwake  na viongozi wengine wa wilaya hiyo katika kikao cha pamoja na mwakilishi wa WFP kituo cha Dodoma Neema Nima Sitta.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu  leo amefanya mazungumzo na mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani(WFP)kituo cha Dodoma Neema Nima Sitta na kujadili changamoto zinazokabili mradi huo ikiwemo baadhi ya wazazi kutochangia pesa kidogo ya kumlipa mpishi  na kununua kuni za kupikia.


Uwepo wa changamoto hizo unatishia mfadhili huyo kusitisha mradi huo wenye  lengo la kusaidia watoto wapate chakula shuleni ili kusaidia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi na kupandisha kiwango cha ufaulu.


Katika kikao hicho Sitta alisema mwaka huu WFP wakishirikiana na Funder Table For Two ya Japan wametenga bajeti ya milioni 692  kwa ajili kusaidia kuleta mahindi,maharagwe na mafuta ya kupikia.


“ WFP na Funder Table For Two wametenga fedha hizo lakini ni wajibu wa wazazi sasa kuchangia malipo ya mpishi na kutafuta kuni,”alisema Sitta.


Alisema wao wanachofanya kwa sasa ni kuendelea kusaidia shule ziweze kulima mashamba ya chakula na mbogamboga ili baadae mradi ukiondolewa basi waweze kujitegemea na watoto wasikose chakula shuleni.


Kwa upande wake Mtaturu akizungumza katika kikao hicho aliahidi kama wilaya  kusimamia wazazi kutatua changamoto hizo ili watoto waendelee kupata chakula shuleni huku akisisitiza  fedha zinazohusu elimu kupelekwa moja kwa moja  shuleni ili kuondoa mwanya wa pesa kutumika kwa matumizi yasiyokusudiwa.


Aliwashukuru wafadhili kwa kuendelea na ufadhili huo licha ya mradi huo kutakiwa kuisha april  mwaka huu.


“kwa niaba ya wilaya nawashukuru sana wafadhili WFP  wakishirikiana na Funder Table for two kutoka Japan kwa kukubali kuendelea na mradi huu hadi December 2017 tofauti na awali ambapo ulikuwa uishe April 2017,”alisema Mtaturu.


Mradi huo unafadhili shule 24 katika Wilaya hiyo ambapo moja ya lengo lake ni kuongeza kiwango cha ufaulu mashuleni ambapo  mwaka jana 2016  wilaya imepandisha kiwango cha ufaulu wa darasa la saba kwa asilimia 71.9 kutoka asilimia  68.5 mwaka 2015.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania