CURRENT NEWS

Thursday, January 19, 2017

RC NDIKILO ATEKELEZA MAELEKEZO ALIYOPEWA NA WAZIRI MKUU MAJALIWA


Mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo, akizungumza na wakazi wa kijiji cha Umwe,Rufiji,baada ya kufungua rasmi zoezi la uvunaji wa mazao ya misitu endelevu wilayani hapo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Rufiji
Mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo, amefungua rasmi zoezi la uvunaji wa mazao ya misitu endelevu katika wilaya za Rufiji na Kibiti ikiwa ni maelekezo kutoka kwa waziri mkuu Kassim Majaliwa.


Aidha waziri mkuu huyo,ameuagiza uongozi huo wa mkoa ,kuwasimamisha kazi baadhi ya watendaji waliokuwa wakisimamia kazi hiyo kwa tuhuma za kutofuata taratibu.

Awali zoezi hilo lilisimamishwa na waziri mkuu huyo, wakati alipofanya ziara wilayani hapo septemba 26 mwaka 2016 kutokana na kubaini ukiukwaji wa taratibu za sheria za nchi zilizokuwa zikifanywa na baadhi ya watendaji wa halmashauri hizo .

Barua hiyo imetaka taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi yao jambo ambalo halmashauri ya wilaya ya Rufiji imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya watumishi hao.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Umwe ,wilayani Rufiji ,mhandisi Ndikilo, alisema kufunguliwa kwa zoezi hilo kunaenda sambamba na uzingatiaji wa sheria kanuni na taratibu za serikali na kama itabainika kuna watu watakaokwenda kinyume watawajibishwa.

Alisema serikali itahakikisha misitu yote inalindwa ili iwe endelevu na kuwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Kama kuna mtu anayedhani kuwa ni mali yake akaitumia kinyume na taratibu anajidanganya,lazima tutekeleze agizo la waziri mkuu ,sasa ameruhusu kwa kuweka masharti ya uzingatiaji wa sheria naomba ushirikiano katika utekelezaji huo na si vinginevyo”alisema.


Mhandisi Ndikilo, aliwaonya viongozi wa vijiji hususan watendaji wa vijiji kuacha kijitabia cha kujihusisha na vitendo vya uvunaji haramu wa mazao ya misitu .
Alieleza kuanzia sasa hatosita kuwafukuza kazi mara moja kwa wale watakaojulikana kwenda kinyume na taratibu zilizopo.

Nae mtendaji mkuu wa wakala wa huduma za misitu nchini ,profesa Dos Santos Silayo, alisema kuwa ili kufikia malengo juu ya kulinda misitu kunahitajika ushirikiano baina ya wananchi na watendaji wa serikali.

Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo alibainisha kwamba,kipindi ambacho serikali ilisimamisha zoezi la uvunaji wa mazao ya misitu alikuwa na wakati mgumu kwa wananchi.

Alisema baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo walikuwa wakimsumbua kumuomba kufunguliwa kwa zoezi hilo na sasa anashukuru ombi lao limeitikwa.

Njwayo alisema wananchi wapo pamoja na serikali kwa kufuata taratibu zinazotolewa juu ya uvunaji endelevu wa misitu licha ya kuwepo baadhi yao ambapo wilaya inaendelea kuwadhibiti.

Mkazi wa kijiji cha Umwe Andrea Iranga, aliuomba uongozi wa mkoa, kuangalia namna ya kuwasaidia ili kuwaletea chakula watakachonunua kwa gharama nafuu kwa kuwa wanakabiliwa na upungufu wa chakula unaotokana na hali ya ukame .
Mkuu wa mkoa wa Pwani,aliwatoa shaka wananchi wenye adha hiyo, na kudai serikali iko makini na sasa baa la njaa hakuna nchini.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania