CURRENT NEWS

Monday, January 9, 2017

TAARIFA KWA UMMA UTOAJI RUZUKU AWAMU YA TATU KWA WACHIMBAJI MADINI WADOGO, 16 JANUARI 2017, MPANDA.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA NISHATI NA MADINITAARIFA KWA UMMA
UTOAJI RUZUKU AWAMU YA TATU KWA WACHIMBAJI MADINI WADOGO, 16 JANUARI 2017, MPANDA.
Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) itatoa Ruzuku ya  jumla ya Shilingi Bilioni 7.481 kwa Wachimbaji Madini Wadogo 59 ambapo kiwango cha juu cha Ruzuku kwa Kikundi/Mtu binafsi kikiwa ni  Shilingi Milioni 210.
Hafla ya utoaji wa Ruzuku hiyo itafanyika siku ya Jumatatu , tarehe 16  Januari 2017, Mjini Mpanda mkoani Katavi, Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim  M. Majaliwa (Mb.).
Fedha za Ruzuku kwa kila Mnufaika, zitatumika kununua vifaa vya kuchimbia au kuchenjulia madini ambapo kabla ya kukabidhiwa vifaa hivyo, wanufaika hao watapata mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya ruzuku yatakayotolewa na Wizara ya Nishati na Madini tarehe 15 Januari, 2017 Mjini Mpanda.
Miradi 59 itakayopata ruzuku hiyo, ndiyo iliyoshinda kati ya miradi 592 ya uchimbaji madini mdogo iliyokuwa kwenye ushindani.. Waombaji wengine ambao maombi yao hayakushinda watajulishwa kwa Barua.
Wizara ya Nishati na Madini ilianza mchujo wa kuwapata Washindi tangu Mwezi Julai 2016, kwa kuwashirikisha , Viongozi wa Wachimbaji Madini Wadogo wa mikoani (REMA’s),Viongozi wa Kitaifa  (FEMATA) pamoja na Viongozi wa Wachimbaji Madini Wanawake (TAWOMA).
Majina ya wanufaika wa Ruzuku awamu ya tatu  pia yanapatikana kwenye Tovuti ya Wizara: www.mem.go.tz pamoja na Ofisi Za Madini Za Kanda.
Imetolewa na,
                                        

Prof. Justin W. Ntalikwa

KATIBU MKUU
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania