CURRENT NEWS

Tuesday, January 17, 2017

VIGWAZA YAPOKEA CHAKULA CHA MSAADA/VIJIJI VYA MBWEWE VYASUSIA


Na Mwamvua Mwinyi,Vigwaza
KIJIJI cha Vigwaza,Chalinze wilayani Bagamoyo,kimepokea kg 1,299 za mahindi ya msaada kutoka halmashauri ya Chalinze ambazo zimeelekezwa kugawiwa kwenye kaya 240 badala ya 1,152 zinazohitaji msaada kijijini hapo.
Akizungumzia suala hilo,wakati wa zoezi la ugawaji wa chakula hicho kwa walengwa,mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Vigwaza,Ramadhani Kirumbi,alisema msaada huo hautoshelezi.
Alisema wamepokea mahindi kg 1,299 ambapo kg 99 zilitakiwa zigawiwe kwenye kaya tatu zisizo na uwezo wa kununua mahindi na kg 1,200 zigawiwe kwenye kaya 240.
Kirumbi alisema ukitoa kaya tatu zinazotakiwa kupata bure mahindi hayo,zinabakia kaya 1,149 hivyo kwa kilo walizopokea kila kaya ingepata kilo moja ambayo haitoshelezi mahitaji.
“Maelekezo tuliyopata tulitakiwa kugawa kwa kaya 240 pekee badala ya 1,152 zilizokuwepo kwenye tathmini kijijini hapa ,hivyo niliamua kuitisha mkutano wa kijiji na kufanya mchanganua kwa kuchagua kaya zilizopigiga kabisa na kupata kaya ambazo tunazipa kilo 3 badala ya moja”alisema.
Aidha Kirumbi alisema,wamelazimika kufanya mchanganua na kukata baadhi ya kaya zenye uwezo wa kula japo mlo mmoja kwa siku ili kupata kaya chache zenye mahitaji zaidi.
Hata hivyo alibainisha ,wananchi wengi wanalalamika kukosa msaada huo wa mahindi.kutokana na utaratibu wa halmashauri na wilaya ni kugawa mahindi hayo kwa kaya 240 pekee ili kupata kilo moja moja.
Mwenyekiti huyo alisema kiukweli hazitoshelezi kwani kilo moja ya mahindi huwezi kutumia hata kwa wiki moja hivyo hali bado sio shwari.
Kirumbi alifafanua,dhamira ni kupata tani 20 kwenye kijiji chake kwa kaya 1,152 ambazo hazina chakula ili kila kaya ipate kilo 50 zitakazowasaidia kustahimili kwa miezi mitatu ijayo huku wakiendelea kujipanga kwa kilimo .
Alisema baadhi ya wananchi hasa wa pembezoni wamekosa chakula kwa miaka miwili mfululizo kulingana na uhaba na mvurugano wa mifugo kuingizwa kiholela kulisha mazao yanayolimwa.
Nae diwani wa kata ya Vigwaza,Mohsin Bwarwani,aliishukuru serikali kwa msaada walioupata .
Alisema atasaidia kulipia mahindi ya kaya zinazotakiwa kulipia sh.50 kwa gharama ya kilo moja ya mahindi ili kuwaondolea makali ya kwenda kusagisha huku wakiwa na shida.
Bwarwani aliwaasa wafugaji kuacha kufuga kiholela badala yake wafuge kisasa ili kuondokana na mifugo kula mazao ya wakulima na kuwasababisha kukosa chakula.
Tausi Ally(70)alisema alikuwa akishindia uji lakini kwasasa licha ya kupata kilo tatu za mahindi akisaga atapata unga utakaomsaidia kula japo kwa siku tatu.
Aliishukuru serikali kwa msaada huo na kuomba isichoke kuwasaidia wananchi wake ambao kiukweli katika baadhi ya maeneo hasa ya vijijini wanateseka .
Fatuma Teua yeye ni kati ya waliokosa msaada huo angali akiwa na shida ya chakula,”aliiomba serikali kufanya tafiti ili kubaini kama kweli hakuna wasio na akiba ya chakula mfano,maeneo ya Chalinze na Bagamoyo,iwasaidie kwani ikumbuke maeneo mengi yalivamiwa na mifugo huku wakulima wamekuwa hawana ziada ya chakula na akiba hakuna .
WAKATI huo huo baadhi ya wakazi wa vijiji vya  mbwewe na Kunduchi kata ya Mbwewe wamekataa msaada wa mahindi ya msaada kutokana na kuwa na kaya zaidi ya 1,000 sawa na wakazi 20,000 huku wakipokea tani moja na kilo 65 pekee.
Mkazi wa Mbwewe Chamwile,alisema chakula hicho hakitoshelezi kwani kwa mgawanyo kila mmoja angepata punje ya mahindi.

Baadhi ya wakazi wanaeleza ni bora wakabakia kula maembe na maji ili waishi kuliko kukubali punje za mahindi .
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania