CURRENT NEWS

Friday, January 27, 2017

WAZIRI LUKUVI ATOA HATI 810 ZA ARDHI KWA WANAKIJIJI MKOANI IRINGA

Wakazi wa Kijiji cha Kinywang’anga Mkoa wa Iringa wakiwa na hati zao za umiliki wa ardhi mara baada ya kukabidhiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi (aliyevaa miwani) akifuatiwa na Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) Ndugu David Thompson na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Richard Kasesela.
Baadhi ya hati miliki za ardhi zikiwa zinaandaliwa ili kugawiwa kwa wananchi wa Kijiji cha Kinywang’anga Mkoani Iringa.
Ndugu Yohanes Keng’ena na Mkewe Elizabeth Makang’olo wakipokea hati miliki ya ardhi kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi.
Bibi Catherine Abdallah akipokea hati miliki ya ardhi kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi.
Ndugu Petro Wilson na Mkewe Leila Mlawa wakipokea hati miliki ya ardhi kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi akiongoza ukataji utepe katika ufunguzi wa masijala ya ardhi ya kijiji cha Kinywang’anga Mkoa wa Iringa.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi akiongoa na wakazi wa Kijiji cha Kinywang’anga Mkoani Iringa.
Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) Ndugu David Thompson akiongoa na wakazi wa Kijiji cha Kinywang’anga Mkoani Iringa.
Moja ya shamba la mkazi wa Kijiji cha Kinywang’anga Mkoani Iringa.



Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi amewakabidhi hati miliki 810 za ardhi kwa wananchi wa Kijiji cha Kinywang’anga kilichipo Mkoani Iringa.

Wananchi hawa wamekabidhiwa hati hizo za umiliki wa ardhi baada ya kupimiwa maeneo yao ya viwanja na mashamba wanayoyamiliki na kuandaliwa hati miliki ambazo walikabidhiwa na Waziri wa Ardhi Mheshimiwa William Lukuvi kijijini hapo.

Katika tukio lingine Mheshimiwa William Lukuvi amezindua masijala ya ardhi ya kijiji cha Kinywang’anga Mkoa wa Iringa ili kuboresha huduma ya utoaji na uhifadhi wa hati miliki za ardhi.

Akizungumza na wakazi wa Kijiji hicho mara baada ya kuwakabidhi hati miliki zao za ardhi na kuzindua baraza hilo Waziri Lukuvi aliwasihi wananchi hao kuzihifadhi na kuzitunza hati zao hizo ili kuepukana na migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi wengi wasio na hati miliki nchini.

Nae Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) walioshirikiana na Serikali kuwezesha uandaaji wa hati miliki hizo Ndugu David Thompson amemshukuru Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi kwa kuja na kuwakabidhi Wananchi hati hizo na kuwaombaa Wananchi kuzitumia kwa maendeleo yao.

Wananchi wa Kijiji cha Kinywang’anga wamemshukuru Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi pamoja na shirika la USAID linaloendesha mradi wa ‘Tanzania Land Tenure Assistance’ kwa kuwaaezesha kupata hati hizo maana ilikuwa kero kubwa katika kata yao.

Aidha, Waziri wa Ardhi ametoa hati miliki hizo ili kutekeleza Programu ya Kitaifa ya kupima na kumilikisha ardhi na kuzuia migogoro ya ardhi yenye lengo la kutekelezwa nchi nzima. Utekelezaji huu utahusisha kuhakiki mipaka ya Mitaa na Vijiji pamoja na maeneo mengine yote nchini na kupima kila kipande cha ardhi kwa lengo la kumilikisha ardhi hiyo kwa wananchi, taasisi na Kampuni.

Sambamba na hilo, Matangazo ya Serikali yanayotambulisha mipaka ya mikoa, Wilaya, Hifadhi za Taifa na vijiji yatafanyiwa marekebisho baada ya mipaka yote nchini kuhakikiwa na kukamilika.

Aidha mpango huu unalenga kuwaunganisha wadau wa sekta ya ardhi katika kupanga, kupima, na kumilikisha ardhi nchini na kuweka kumbukumbu za vipande vya ardhi ili kuongeza thamani ya ardhi na kuondoa migogoro ya ardhi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Serikali ya awamu ya tano imeweka adhma ya kumaliza migogoro ya ardhi iliyopo sasa na kuzuia kasi ongezeko la migogoro ya ardhi ndani ya miaka mitano kwa kuandaa mpango kabambe wa matumizi na usimamizi wa ardhi kwa kuharakisha na kurahisisha upatikanaji wa hati za umiliki wa viwanja na mashamba.

Na Hassan Mabuye (Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Ardhi)
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania