CURRENT NEWS

Sunday, January 29, 2017

ZAIDI YA WATU 90 WAPOTEZA MAISHA KUTOKANA NA MVUA KALI NCHINI THAILAND


Kituo cha kuzuia na kupunguza majanga ya kimaumbile nchini Thailand kimetangaza kuwa, kwa akali watu 90 wamepoteza maisha yao kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kali zinazoendelea kunyesha katika mikoa 12 ya kusini mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na kituo hicho imeinukuu serikali ya Thailand ikisema kuwa, watu hao wamepoteza maisha kutokana na mvua hizo na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kubwa kutokana na ongezeko la mafuriko, mawimbi makali ya bahari na kuendelea kunyesha mvua. Kituo cha kuzuia na kupunguza majanga ya kimaumbile nchini Thailand kimetangaza kuwa, hadi sasa mikoa saba ya kusini mwa nchi hiyo bado ina hali mbaya.
Namna ambavyo vijiji vimemezwa na maji Thailand 
Kwa mujibu wa ripoti hiyo jumla ya watu laki nane wameathiriwa na mvua hizo ambazo bado zinaendelea kunyesha. Hii ni katika hali ambayo kituo cha utabiri wa hali ya hewa kimetabiri kunyesha mvua kali ambazo zitashadidi zaidi katika maeneo ya kusini kuanzia siku ya kesho Jumapili na kuendea kuyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi. Utabiri huo pia umetahadharisha juu ya ongezeko la mawimbi makubwa yenye mwinuko wa zaidi ya mita mbili hadi tatu ambayo yatayakumba maeneo ya pwani ambayo hutembelewa sana na watalii.
Miji ya kusini mwa Thailand iliyomezwa na maji
Kufuatia hali hiyo, serikali imetuma maelfu ya askari kwa ajili ya kuwaokoa maelfu ya wakazi wa vijijini walivyozingirwa na mafuriko sanjari na kukarabati barabara na madaraja katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania