CURRENT NEWS

Wednesday, February 15, 2017

DC MTATURU AAGIZA KUKAMATWA MWENYEKITI WA KIJIJI SAKAA KWA KUFUJA FEDHA.

 
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akimsikiliza Mtendaji wa Kijiji cha Sakaa Robert Soah(aliyesimama) akisoma taarifa ya kijiji katika mkutano wa hadhara. 

                Wananchi wa kijiji cha Sakaa wakisikiliza kwa makini yanayoendelea katika mkutano wa kijiji.
      Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akizungumza na wananchi  katika mkutano     wa Kijiji cha Sakaa.
..........................................................................................
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu ameagiza kukamatwa kwa mwenyekiti wa kijiji cha Sakaa kilichopo kata ya Misughaa wilayani humo Shabani Rajabu(CHADEMA) na kuhojiwa kutokana na kutuhumiwa kufuja fedha na matumizi mabaya ya madaraka.
                 
Agizo la mkuu huyo wa wilaya amelitoa leo kwenye mkutano kijijini hapo mbele ya wananchi kufuatia kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi ya kutokuwa na imani na mwenyekiti wao.

Akizungumza katika mkutano huo, Omari Musa ambaye ni mmoja wa wanakijiji alisema wamekuwa na malalamiko mengi dhidi ya mwenyekiti wao kutokana na kufanya mambo kinyume na taratibu bila ya kushirikisha wenzie ikiwemo na kutosoma mapato na matumizi.

“Mwenyekiti amefanya ufujaji wa mapato,amekuwa akikusanya  ushuru wa mawe,mchanga,rasilimali ya misitu,faini za usafi wa mazingira amekuwa anapokea yeye na mjumbe wa halmashauri ya kijiji ambae alikuwa katibu wa kamati ya mipango na fedha Nyasi Njiku badala ya kumuachia akusanye afisa mtendaji,”alisema mwananchi huyo.

Kwa upande wake, Hamis Sanka ambaye ni mmoja wa wajumbe wa halmashauri ya Kijiji akizungumza katika mkutano huo alisema wao kama wajumbe walipoona mambo hayaendi sawa wajumbe wapatao 14 kati ya 23 walijiengua kushiriki vikao.

“Sisi tuliamua kujiengua baada ya kuona malalamiko yamekuwa mengi na mwenyekiti anafanya maamuzi bila ya kutushirikisha na hivyo tuliamua kuleta hoja ya kuitishwa kikao hiki,”alisema mjumbe huyo.

Baada ya kupokea malalamiko hayo,Mkuu wa wilaya huyo aliagiza mwenyekiti huyo ambaye hakuwepo mkutanoni na katibu wa kamati ya mipango na  fedha Nyasi Njiku waripoti kituo cha polisi kesho ili kujua mwenendo wa fedha za umma walizonazo ikizingatiwa hawajasoma mapato na matumizi tangu mwezi machi mwaka jana.

“Naagiza pia vijiji vyote ambavyo havijawasomea wananchi taarifa za mapato wahakikishe wanafanya hivyo na hadi kufikia tarehe 5 mwezi machi niwe nimepata taarifa ya vijiji vya wilaya nzima,”alisema Mtaturu.

Alieleza athari zilizopatikana kutokana na mwenyekiti huyo kushindwa kutimiza wajibu wake kuwa ni pamoja na ujenzi wa darasa katika shule ya msingi kijijini hapo kusimama na jengo la ofisi ya kijiji kutoanza hadi sasa.

Kadhalika, Mtaturu aliunda tume ambayo ilipewa jukumu la kuambatana na mkaguzi wa mahesabu wa ndani ili kubaini ni kiasi gani cha fedha kilichofujwa na taarifa aipate ndani ya wiki moja ili wananchi wajulishwe waweze kuendelea kushiriki shughuli za maendeleo.


Baada ya yote hayo wananchi walimchagua ndugu Hamisi Sanka kuwa mwenyekiti wa muda wa kijiji hicho baada ya kupiga kura 355 kati ya 360 walizopiga wananchi kwa ajili ya kumuondoa mwenyekiti anayetuhumiwa.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania