CURRENT NEWS

Sunday, February 12, 2017

DC MTATURU AWATAKA WANARIADHA MKOA WA SINGIDA KUJIWEKA TAYARI KUKABILIANA NA MASHINDANO YA NYIKA TAIFAMkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akisalimiana na baadhi ya wanariadha wa mkoa wa Singida walioweka kambi katika kijiji cha Puma wilayani humo  wakijiandaa na mashindano ya Nyika Taifa yatakayofanyika mjini Moshi.


Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu katikati akizungumza na wanariadha hawapo pichani alipowatembelea kambini 
 Mkuu wa wilaya ya Ikungi katikati akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wilaya hiyo kulia kwake ni katibu wa Chama cha Riadha mkoa wa Singida  Benno Msanga,Katibu wa CCM wilaya Alluu Segamba, Mwenyekiti wa Chama Cha Riadha mkoa Mwalimu Itembe na kushoto kwake ni Katibu Tawala Wilaya Winfrida Funto,Mwenyekiti wa CCM Kata ya Puma  Tano Likapakapa na afisa mtendaji wa kata ya Puma.
                     .........................................................................................................................
MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu leo ametembelea kambi ya wanariadha timu ya mkoa iliyopo katika kijiji cha puma wilayani humo huku akiwahimiza kuzingatia mafunzo wanayopewa na wakufunzi wao ili kujiweka tayari katika mashindano ya Nyika Taifa yanayotarajiwa kufanyika februari 18 mjini Moshi.

Wanariadha hao 15 wanatarajia kuchuana katika mashindano  ya Nyika Taifa yanayofanyika ili kutafuta timu ya Taifa itakayoshiriki mashindano ya Nyika ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika mjini  Kampala nchini Uganda mapema mwezi machi mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kufika kambini hapo Mtaturu amesema muhimu kwao ni kuzingatia maelekezo wanayopewa na walimu wao  na kuyafanyia kazi ili hatimaye wapate nafasi ya kuliwakilisha Taifa katika mchezo wa riadha.

"Kama serikali tutaendela kuwasaidia ili kuweza  kutatua changamoto zote zinazoikabili kambi ikiwemo chakula,malazi na dawa kwa ajili ya maumivu madogo madogo mnayoyapata kwenye mazoezi"alisema Mtaturu.

Aliwataka kutumia vizuri nafasi hiyo adhimu kwao na kwa mkoa kwa ujumla ili kuuletea ushindi mkoa na baadae Taifa.

Kwa upande wake katibu wa chama cha riadha mkoa Benno Msanga alisema  kambi inaendelea na wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanapata ushindi.

"Kama mnavyoona wanariadha wapo katika hali nzuri tayari kutoa ushindani mkali kwenye mashindano ya mjini Moshi na rekodi zao ni nzuri sana mpaka sasa"alisema Msanga.

Alimshukuru mkuu wa wilaya Mtaturu kwa kuwa karibu na kambi ya riadha toka  ianze tarehe 24 januari kwa kutoa  huduma mbalimbali.

Mkoa wa singida ni chimbuko la wanariadha wengi waliowahi kusikika kimataifa mmojawapo ni Aliphonce Alex Simbu aliyeshinda Medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Mumbai Marathon yaliyofanyika chini India  mapema mwezi januari 2017,Simbu ni mzaliwa wa kijiji cha Mampando wilayani Ikungi. 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania