CURRENT NEWS

Wednesday, February 15, 2017

DK.KAWAMBWA -MCHAGUENI SWEDY TUSIMAMIE TATIZO LA MAJI /UMEME KITONGOJI CHA MAGOMENI B

 Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, dk. Shukuru Kawambwa, akizungumza kwenye mkutano wa kampeni, kumnadi mgombea nafasi ya mwenyekiti kupitia CCM kitongoji cha Magomeni B, Rajabu Swedy.

Meneja kampeni uchaguzi mdogo kitongoji cha Magomeni B (CCM)alhaj Abdul Zahoro ,akimkaribisha mbunge wa jimbo la Bagamoyo, dk. Shukuru Kawambwa kumnadi mgombea kupitia CCM Rajabu Swedy. (picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
MBUNGE wa jimbo la Bagamoyo, mkoani Pwani, dk. Shukuru Kawambwa, amesema anaendelea kuivalia njuga changamoto ya maji inayokabili baadhi ya maeneo jimboni hapo ikiwemo kitongoji cha Magomeni B.
Aidha ameeleza jitihada alizozifanya kuhakikisha vijiji na vitongoji vinavyokabiliwa na changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme ,vinaingizwa katika awamu ya III ya umeme vijijini (REA) .
Dk. Kawambwa aliyasema hayo, wakati akimnadi mgombea wa nafasi ya mwenyekiti kitongoji cha Magomeni B ,Rajabu Swedy katika kampeni zinazoendelea kufanyika.
Alisema yeye ataweza kusimamia na kutatua changamoto mbalimbali kwa kushirikiana na viongozi kutoka CCM badala ya wapinzani.
"Ni mengi nayafanya na mengine nikiendelea kuyafuatilia katika idara husika hivyo msifanye makosa kuwapa ridhaa vyama vya upinzani bali mchagueni Swedy kuwa mwenyekiti wenu"alisema dk. Kawambwa.
Dk. Kawambwa alisema endapo atachaguliwa mtu kutoka vyama vya upinzani atashindwa kufanya nae kazi kirahisi.
Hata hivyo alieleza kwamba, kwasasa mabomba makuu ya usafirishaji maji yameshalazwa na mtandao wa mabomba ukiendelea kutandazwa .
Alisema zoezi hilo litakapokamilika itasaidia kuondoa adha ya maji jimboni humo.
Dk.Kawambwa alisema ,anashirikiana na viongozi mbalimbali wa vitongoji, vijiji, madiwani kufuatilia tatizo hilo,kwa kuzungumza na wizara husika na dawasco kujua hatua zinazoendelea .
Kuhusu nishati ya umeme alisema changamoto hiyo itakuwa historia baada ya vitongoji vyote kuingizwa katika awamu ya tatu ya REA .
Nae katibu wa chama cha mapinduzi (CCM),Kombo Kamote, alisema wananchi wa kitongoji cha Magomeni B wamuamini Swedy kwani ana sifa na uwezo wa kuwaongoza.
Kamote aliwaasa wasijaribu kuchagua vyama visivyo na sera makini.
Diwani wa kata ya Magomeni, Mwanaharusi Jarhuf, alisema halmashauri ya wilaya hiyo, imepanga kujenga kisima kikubwa kitakachokuwa na uwezo wa kulisha maeneo mengi ya wilaya ikiwemo Magomeni B.
Mwanaharusi alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwatua ndoo kichwani akinamama .
Meneja wa kampeni za uchaguzi mdogo katika kitongoji hicho, alhaj Abdul Zahoro, aliwasihi wananchi kujitokeza februari 19 kwenda kupiga kura.
Alhaj Zahoro alisema wasihadaike, wasidanganywe bali kiongozi makini ni Swedy kutoka CCM.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania