CURRENT NEWS

Saturday, February 11, 2017

EBRAHIM-KUTUPA VICHANGA/KUTELEKEZA WATOTO CHANZO CHA ONGEZEKO LA WATOTO YATIMA

 Mwenyekiti wa asasi ya amazing step for children foundation,Daisy Ndege ,akionekana amembeba mtoto wa miezi miezi minne(Mercy Ndege) anaelelewa katika kituo cha parmanent glory home ambacho kipo chini ya asasi hiyo,ambapo mtoto huyo aliokotwa pori la Chalinze akiwa na umri wa siku moja.


Katibu mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Time To Help,Ibrahim Salum Ebrahim,akikabidhi misaada ya vyakula mbalimbali kwa mlezi wa kituo cha parmanent glory home,Daisy Ndege.

Story/picha na  Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
IMEELEZWA kuwa kitendo cha kutupa vitoto vichanga na kutelekeza watoto ni moja ya chanzo kinachochangia ongezeko la watoto yatima ndani ya jamii.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya akinamama wametakiwa kujipanga kabla ya kuchukua maamuzi ya kubeba mimba ili kujiepusha na vitendo hivyo baada ya kuzaa.

Aidha wadau na jamii imeombwa kushirikiana kwa pamoja kuwezesha vituo vinavyojishughulisha na kusaidia watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu ili waweze kutoa huduma na malezi yaliyo bora .

Hayo yalielezwa na katibu mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Time To Help) Ibrahim Salum Ebrahim,mara baada ya kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Parmanent Glory Home kilichopo kata ya Yombo wilayani Bagamoyo.

Alisema akinamama na wasichana ni lazima wamuogope mungu kwa hilo,kwani kutelekeza watoto wakiwa wadogo na kutupa vichanga ni ukatili kwa watoto .

“Wengi wanasingizia maisha magumu na ugomvi kwenye ndoa ndio sababu inayowasababisha kutupa watoto na kuwatelekeza ,muwe na uchungu,ukizingatia umebeba mimba kwa miezi tisa na kuhangaika nayo”alisema Ebrahim.

Ebrahim alielezea kwamba,wameguswa na tukio la mtoto kichanga aliyetupwa huko pori la Chalinze mita tano kutoka barabarani ambae amepelekwa katika kituo cha permanent Glory Home kulelewa.

Alisema mtoto huyo kwa sasa ana miezi minne,hivyo ieleweke kuchukua jukumu la kulea kichanga na watoto wanaotelekezwa inahitaji moyo na watu hao wanatakiwa kuungwa mkono.

Ebrahim alisema shirika hilo,limeamua kusaidia mchele,unga wa sembe na wa ngano,maharage,mafuta ya kupikia,maziwa,juice,biscuit na vyakula vingine vyote vikiwa vimegharimu sh.400,000.

Hata hivyo alisema shirika hilo pia linajishughulisha na uchimbaji visima nchini,na kwasasa wanaanza mchakato wa kuchimba visima vitano kata ya Yombo ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa maji.

Ebrahim alieleza kuwa,walipelekewa maombi na mbunge wa jimbo la Bagamoyo,dk.Shukuru Kawambwa kwenda kusaidia kuchimba visima kwenye maeneo mbalimbali jimboni hapo ambapo wameanza na kata hiyo.

Nae mlezi wa kituo hicho cha kulelea watoto yatima kilichopo chini ya asasi ya amazing step for children foundation,Daisy Ndege ,alisema kituo hicho kilianza mwaka 2014 na hadi sasa kinalea watoto yatima 24 .

Alisema asasi hiyo licha ya kujishughulisha na ulezi wa watoto,pia inatoa elimu ya afya,uzazi,kwa vijana,masuala ya ujasiriamali,inatoa elimu rika na inahudumia watoto wa majumbani wenye mazingira magumu.

Daisy alifafanua ,kituo hicho kinajiendesha kwa kutumia wadau wa ndani,taasisi na mbunge wa jimbo hilo,lakini bado hawajapata wafadhili wa kudumu.


Katibu wa mbunge wa jimbo la Bagamoyo,Magreth Masenga,alisema dk,Kawambwa alizungumza na shirika la Time To Help kuangalia namna ya kusaidia kupunguza tatizo la maji hasa maeneo ya vijijini .

Kwa mujibu wa Magreth ,mbunge huyo anaendelea kushirikiana na mashirika ,wadau na taasisi mbalimbali kutatua changamoto zinazolikabili jimbo hilo,ikiwemo kusaidia makundi maalum,watoto yatima,afya ,elimu na maji.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania