CURRENT NEWS

Monday, February 27, 2017

HALMASHAURI YA CHALINZE YAPITISHA BIL.42 KWA MWAKA 2017/2018

 Diwani wa kata ya Lugoba, Rehema Mwene, akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Chalinze.
 Baadhi wa madiwani halmashauri ya Chalinze wakisikiliza jambo katika baraza la madiwani lililopitisha makisio ya bajeti 2017/2018
Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze, Saidi Zikatimu,akizungumza katika baraza la madiwani lililopitisha makisio ya bajeti 2017/2018.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
HALMASHAURI ya Mji wa Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani imepitisha mpango wa bajeti yake ya sh.bil 42 kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze ,Said Zikatimu wakati wa kikao cha bajeti kilichofanyika Lugoba.
Alieleza kwamba,hayo ni mapendekezo ambayo baadae yatapelekwa kwenye kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) ili kuyapitisha kisha kupitishwa bungeni.
Zikatimu alisema kuwa, kati ya fedha hizo zitakazotokana na mapato ya ndani ni bil 4.6, fedha za miradi ya maendeleo bil 8.8 ndizo zitakazotumika kwa kipindi hicho.
Mwenyekiti huyo alisema,wanatarajia kukusanya fedha hizo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa ushuru mbalimbali.
"Hadi kufikia desemba mwaka 2016 tulikuwa tumekusanya asilimia 59 ambayo ni mapato ya ndani na tunatarajia kufikia asilimia 100 itakapofika mwisho wa mwaka wa bajeti."
"Baadhi ya matumizi tunayotarajia ni idara ya elimu ya msingi ambayo itatumia kiasi cha sh.mil 400 na miradi, mishahara." alisema Zikatimu.
Zikatimu alifafanua kwamba,matumizi mengine ni zaidi ya sh.bil 2, idara ya maji mil 250, idara ya afya mil 200, utawala mil 302 ,ugavi mil 100, ujenzi mil 150, biashara mil 100, maendeleo ya jamii mil 460 na  mipango mil.420.
Nae mkurugenzi wa halmashauri ya Chalinze,Edes Lukoa alisema wameendelea kuboresha ukusanyaji wa mapato ikiwemo kununua mashine za EFD na kuachana na mfumo wa ukusanyaji wa kutumia risiti za kawaida ambao ulikuwa na uvujaji wa mapato mengi.
Alisema wamenunua mashine hizo kama ilivyokuwa mapendekezo ya baraza la madiwani lililopita ambao kwa kauli moja wameridhia kununuliwa mashine za kutosha ili kuongeza mapato.
Lukoa alibainisha wataendelea kudhibiti uvujaji na kuongeza vyanzo vya mapato ambavyo vimependekezwa ili kufikia malengo.
Diwani wa kata ya Lugoba Rehema Mwene alisema baadhi ya vyanzo kikiwemo cha mchanga bado hakijadhibitiwa vizuri.
Aliomba udhibiti uongezwe ili kuongeza mapato zaidi ya ilivyosasa kwani bado kunaulegelege katika kudhibiti baadhi ya vyanzo.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania