CURRENT NEWS

Saturday, February 4, 2017

KUELEKEA KUZALIWA KWA CCM KATIBU MAKILAGI AWAASA WANACCM KUCHAGUA VIONGOZI BORA KATIKA UCHAGUZI WA NDANI YA CHAMA.


 Katibu mkuu wa UWT Mama Makilagi akiwa na mbunge wa viti maalum na mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UWT Taifa Zainab Mwamwindi wakipokea zawadi walizopewa na wanachama wa Jumuiya hiyo wilayani Mpwapwa.

  Katibu Mkuu wa UWT Taifa Amina Makilagi akimsalimia mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya wilaya ya Mpwapwa baada ya kutoa misaada kwa wagonjwa hao.

 Katibu Mkuu wa jumuiya ya Wanawake Tanzania(UWT)Amina Makilagi akizungumza na akina mama wanaosubiri kujifungua waliopo katika kituo cha Chigonela kilichopo katika hospitali ya wilaya ya Mpwapwa alipoenda kuwapa misaada mbalimbali ikiwa ni maadhimisho ya miaka 40 ya kuzaliwa CCM iliyoratibiwa na jumuiya hiyo.
Katibu Mkuu wa UWT Taifa Amina Makilagi akipanda mti katika ofisi za CCM wilaya ya Mpwapwa alipoenda kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 40 yaliyoratibiwa na UWT.

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania(UWT)Amina Makilagi  amewataka wanawake nchini kutumia maadhimisho ya miaka 40 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi(CCM)kujitafakari na kuchagua viongozi bora kwa maslahi ya Chama na Jumuiya katika chaguzi zijazo.
 
Aidha amevitaka vikao halali vya uchujaji muda utakapofika kuchuja majina kwa haki na kutopitisha jina la mgombea yoyote atakayejihusisha na rushwa.
 
Akizungumza na wanachama wa UWT na wana CCM kwa ujumla katika kikao cha ndani wilayani Mpwapwa ikiwa ni katika kuadihimisha miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM  Makilagi alisema mwaka huu chama na jumuiya zake kinaingia katika uchaguzi kwa mujibu wa Katiba,Kanuni na taratibu walizojiwekea hivyo chama kikiwa na viongozi imara ni rahisi kupata viongozi bora na chama kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwama  2020.
 
Alisema kiongozi bora ni yule anayeweka maslahi ya watu na chama mbele bila ya kuyaweka maslahi yake binafsi mbele na pia sio anayetafuta uongozi kwa rushwa.
 
“katika uchaguzi huu tusipochagua viongozi wanaotanguliza maslahi ya watu na chama mbele 2020 tutapata shida,tutumie maadhimisho haya kujitathimini kama unafaa kwa yeyote unayetaka kugombea,”alisema Makilagi.
 
Aliwataka wazazi na walezi wakati wakitafakari miaka 40 ya kuzaliwa CCM wadumishe na kusimamia maadili kwa vijana wao ili kuwaandaa viongozi bora wa kesho.
 
“watengenezeni vijana ili wawe viongozi wa kesho,nataka siku moja nisikie katibu wa UWT Taifa anatoka Mpwapwa au rais anatoka hapa,na hili litafanikiwa kama mtasimamia maadili ya watoto wenu na kuwapa elimu bora,”aliongeza MAKILAGI.
 
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 40 ya CCM alisema nchi imeendelea kuwa ya amani na utulivu,huduma za jamii zimeimarika pamoja na changamoto ambazo chama kimezipitia.
 
Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UWT Taifa ambaye pia ni mbunge wa viti maalum Zainab Mwamwindi aliwataka wakazi wa Mpwapwa kutolala baada ya uchaguzi kupita bali wajiandae kwa uchaguzi mwingine ujao.
 
“mlifanya vizuri katika uchaguzi uliopita lakini hiyo isiwe kigezo cha kulala bali muamke mjiandae kwa uchaguzi ujao lakini kikubwa muwe na subira na uvumilivu,”alisema Mwamwindi.
 
Mmoja wa wana CCM wakongwe mzee John Kasambala Mangula ambaye ni baba mzazi wa makamu mwenyekiti wa CCM bara mzee Philip Mangula akizungumzia miaka 40 ya kuzaliwa CCM alikipongeza chama kwa hatua hiyo na kutoa rai kwa viongozi na wanachama kukienzi na kufuata yale mazuri yaliyofanywa na waasisi wa chama hicho ili chama kiendelee kuwa imara.

Mbali na kuzungumza na wana CCM katibu Makilagi alitumia siku hiyo pia kutembelea wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Mpwapwa na kuwapa zawadi huku akipokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wagonjwa na kuahidi kuzifikisha kwa wahusika kwa ajili ya kutatuliwa
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania