CURRENT NEWS

Friday, February 3, 2017

RC NDIKILO-RUSHWA NI MWIBA UNAOSABABISHA KUKWAMA KWA UTOAJI HAKI 


Picha mbalimbali zikionyesha mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,akiwa pamoja na watumishi,wanasheria na mahakimu katika mahakama ya wilaya ya Kibaha.
(Picha zote na Mwamvua Mwinyi) 
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,amezitaka mahakama,polisi na mawakili kutenda haki kwenye majukumu yao ya kazi pasipo kujihusisha na vitendo vya rushwa ambavyo vinasababisha mlundikano wa kesi.
Aidha amewataka wapelelezi na mawakili wa serikali kuzipa kipaombele kikubwa kesi zinazohusisha waliowapa mimba za utotoni wanafunzi wa kike na unyanyasaji wa watoto kijumla kwa kutoa adhabu kali ili iwe fundisho.
Mhandisi Ndikilo,amewaasa pia kuacha kupiga kalenda kesi bila sababu za msingi suala linalisababisha mashauri na watuhumiwa mahabusu kuchukua muda.
Akizungumza kwenye siku ya sheria nchini katika viwanja vya mahakama ya hakimu mkazi –Kibaha ,alisema vitendo vya rushwa ni mwiba unaorudisha nyuma jitihada za serikali katika kufikia ukuaji wa uchumi.
“Mchakato wa utoaji haki umekumbwa na changamoto ya baadhi ya watumishi wa umma na wasio wa umma kujihusisha na vitendo vya rushwa ,ninawasihi mahakimu,watumishi wa mahakama na wananchi ,kuachana na vitendo hivyo”
Mhandisi Ndikilo,alisema haki ni msingi mkubwa wa ustawi wa jamii na kwa umuhimu huo ,jamii isiyo zingatia misingi ya haki kama ilivyoainishwa katika sura (3)ya katiba ya mwaka 1977,itakumbwa na changamoto nyingi katika kukuza uchumi wake.
Alisema ni wajibu wao kuhakikisha kuna kuwa na kizazi ambacho kinapata mahitaji muhimu yatakayowajenga na kuwaandaa vijana kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Hata hivyo alieleza kwamba,maandalizi hayo ni pamoja na kuhakikisha vijana wanapata fursa ya kutimiza ndoto zao kwa kuwajengea mazingira rafiki ya kutimiza ndoto zao kitaaluma.
“Changamoto kubwa kwasasa katika eneo hili ni baadhi ya watoto wetu waliopo shuleni kupata mimba na hivyo kukatisha dhamira na malengo yao kimasomo na kimaisha”alisema mkuu huyo wa mkoa.
Mhandisi Ndikilo,aliviagiza vyombo vyote vinavyohusika katika mchakato wa kushughulikia wanaowapa mimba watoto wa shule kuwashughulikia ipasavyo kwa kufuata sheria ili kukomesha watu wenye tabia za aina hiyo.
Alieleza ,licha ya kutekeleza wajibu wao kimsingi wa kimahakama katika kutoa haki kwa wakati,lakini anatambua kuna changamoto zinazowakabili ambazo serikali inazifanyia kazi.
Alisema serikali ya mkoa inaendelea kuelekeza wakurugenzi watendaji wa halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya mahakama na nyumba za watumishi wa mahakama kila wanapofanya upimaji kwenye maeneo yao.
Nae hakimu mkazi mwandamizi mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi,Kibaha Elizabeth Nyembele,alisema ushiriki wa wadau ni muhimu ili haki itolewe kwa wakati.
Alielezea kuwa kwa ushirikiano baina ya polisi,vitengo vya asasi zisizo za kiserikali,waendesha mashtaka,mlalamikaji na mshtakiwa na mdai na mdaiwa unaweza kusaidia kutoa haki bila ubaguzi na kwa wakati.
Elizabeth alisema itambuliwe kwamba uwezeshaji wa utoaji haki kwa wakati si wa mahakama pekee bali kwa wadau wanaohusika kushiriki kikamilifu.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania