CURRENT NEWS

Monday, February 6, 2017

UJENZI WA MABWENI NA NYUMBA ZA WALIMU S/SEK NASIBUGANI WAOKOA MAMILIONI YA FEDHA 
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo,akionyeshwa ramani ya ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu zinazojengwa katika shule ya sekondari Nasibugani,kulia ni mkuu wa wilaya ya Mkuranga Gilbert Sanga.

 Mkuu wa mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo,(aliyeinua mkono)
akiangalia ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu zinazojengwa katika shule ya sekondari Nasibugani.

(Picha/Story na  Mwamvua Mwinyi)
HALMASHAURI ya wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani,imeokoa kiasi cha sh.bil moja endapo ingetumia wakandarasi katika ujenzi wa mabweni(5) na nyumba za walimu (5)zinazojengwa shule ya sekondari ya Nasibugani.

Aidha serikali mkoani hapo,imelipongeza jeshi la kujenga Taifa (JKT)Ruvu Mlandizi,Kibaha,kupitia luteni kanal Charles Mbuge,kwa kupelekea vijana 107,wa kujitolea kujenga mabweni na nyumba hizo,kwa gharama nafuu.

Mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,aliyasema hayo,wakati alipotembelea shule hiyo,kwenda kujionea ujenzi huo unavyoendelea.


Alisema hadi sasa ujenzi huo umegharimu zaidi ya mil.178 badala ya bil.moja ambazo zingetumika.

Alieleza  kwamba ,suala la kujitolea ni jambo muhimu ndani ya jamii ili hali kujenga ushirikiano baina ya wananchi,wadau na serikali pasipo kuiachia serikali pekee.

Mhandisi Ndikilo,alisema serikali inatoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne lakini haimaanishi kuona kuna mambo muhimu ya kuchangia wazazi wakashindwa kufanya hivyo.

“Sekta ya elimu bado inakabiliwa na changamoto za miundombinu ikiwemo,upungufu wa nyumba za walimu,madarasa,maabara,mabweni na matundu ya vyoo”

“Lazima tushirikiane kwa pamoja tutafute raslimali watu,fedha,kumaliza matatizo haya,tumevulia nguo maji lazima tuyaoge,hadi kazi hii iishe”alisema mhandisi Ndikilo.

“Na yote haya yanapunguza ufanisi wa kuinua sekta hii ya elimu,na kutatua kwake vinahitaji fedha nyingi ambazo halmashauri haziwezi kumudu peke yake"

Mhandisi Ndikilo,alisema endapo nyumba hizo zikikamilika wataweza kuishi walimu kumi na upande wa mabweni yatakuwa na uwezo wa kulaza wanafunzi si chini ya 800.

Aliwaomba wadau wa kimaendeleo waendelee kujitokeza kusaidia ujenzi huo ili ukamilike mapema .
Nae mkuu wa wilaya ya Mkuranga,Gilbert Sanga alisema pia waziri wa elimu Profesa Joyce Ndalichako, alitoa kiasi cha sh.mil 250 ambazo zinaendelea kutumika kwenye ujenzi huo.
   
Alisema mchakato wa ujenzi wa mabweni na  nyumba hizo za walimu ulianza baada ya wananchi kuchangia zaidi ya mil.nne .


“Halmashauri ilidai imetenga fedha kiasi cha sh. mil 32 kwa bweni moja wanafunzi 48 pekee hivyo tuliungana na kamati ya ulinzi na usalama nao walikubali kuongeza mabweni na mkoa uliunga mkono”alisema Sanga.

Msimamizi wa ujenzi kutoka kikosi cha Ruvu JKT,Mohamed Boko alieleza kazi hiyo, ilipangwa kufanyika kwa miezi miwili lakini imechukua muda .


Mwisho.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania