CURRENT NEWS

Friday, February 3, 2017

WATUMISHI WA MAHAKAMA WAASWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI  Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Watendaji na watumishi mbalimbali wa mahakama (M), Viongozi wa dini,viongozi wengine wa Serikali na kwaya ya IACT Bariadi wakiwa ktk maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini kimkoa mjini Bariadi
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka 

Na Stella Kalinga

Watumishi wa idara ya mahakama wameaswa kufanya kazi zao kwa weledi pasipo kutia unajisi wadau wengine wa mahakama hususani jeshi la polisi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya Mjini Bariadi, chini ya kauli mbiu"UMUHIMU WA UTOAJI WA HAKI KWA WAKATI KUWEZESHA UKUAJI WA UCHUMI".

"Ukikaa Mtaani utasikia huyo hapo alikuwa mwizi akakamatwa akapelekwa polisi akaachiwa, kumbe hawajui kuwa kaachiwa mahakamani aliposhinda kesi lakini mdau wenu mmoja analaumiwa sana, ni vizuri mkafanya kazi kwa weledi ili tafsiri ya wadau wenu kuwa kwenye mtazamo hasi kwa jamii uondoke", alisema.

Mtaka amesema kumekuwa na malalamiko mengi ya wananchi dhidi ya jeshi la polisi hata pale inapotokea mapungufu katika utendaji wa watumishi wa mahakama,  kwa kuwa baadhi yao hawajui kuwa baada ya mtu kupelekwa polisi hupelekwa mahakamani.

Amesema watoa haki wa mahakama wanatambulika kama wasomi (learned brothers and sisters) hivyo, wanapaswa kujiridhisha katika utoaji wa maamuzi yao ili wasiifedheheshe taaluma yao na mhimili wa mahakama kwa ujumla.

Aidha,ameipongeza idara ya mahakama na wadau wengine wakiwemo viongozi wa dini,jeshi la polisi kwa mchango wao wa kubadili taswira ya mkoa huo  katika kushughulikia kesi za uhalifu zikiwemo za kukatana mapanga kwa visasi,mauaji ya vikongwe na mauaji ya albino na kufanya mkoa huu kusikika kwa mema.

Ameongeza kuwa mkoa wa Simiyu umejitambulisha kama mkoa wa tofauti ktk masuala mbalimbali ya kiuchumi na Mhe.Rais amewataka wengine kujifunza Simiyu, hivyo akawataka watumishi wa mahakama kujituma na kutoa haki kwa wakati ili wengine waje kujifunza pia katika utendaji wa Mahakama.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS) ambaye  ni wakili, Polycarp Mtega amesema mambo yanayochelewesha utoaji wa haki kwa wakati ni pamoja na ukosefu wa maadili kwa baadhi ya watoa haki, upungufu wa watoa haki katika mahakama,watuhumiwa kutofikishwa mahakamani toka gerezani kwa misingi ya kisiasa, ukosefu wa mashahidi na kesi kuahirishwa pasipo sababu za msingi.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi(M) Mhe. John Nkwabi amesema Mahakama ya Tanzania imejipanga kuhakikisha wadau wote wanapata haki zao kwa wakati ili wajikite katika shughuli za kiuchumi badala ya kupoteza muda mwingi mahakamani, ambapo ameeleza kuwa jumla ya kesi 692 zimesikilizwa kwa mwaka 2016, pamoja na upungufu wa mahakimu uliopo mkoani Simiyu.

Nkwabi ametoa wito kwa wananchi wenye kesi kufika mahakamani kila wanapohitajika badala ya kusubiri kutumiwa hati za kuitwa mahakamani.

Siku ya sheria nchini huadhimishwa kila wiki ya kwanza ya mwezi Februari kila mwaka.

 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania