CURRENT NEWS

Sunday, March 5, 2017

BARAZA LA MADIWANI MANISPAA YA UBUNGO LAPITISHA KWA 100% BAJETI YA ZAIDI YA BILIONI MIA MOJA

Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam wakiwa katika kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 (Picha zote na Nassir Bakari)
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 kulia kwake ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob
Kushoto ni Muweka hazina wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Bi Jenny Machicho, Afisa utumishi Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ally Juma Ally, na Mchumi wa Halmashauri ya manispaa ya Ubungo Yamo Wambura wakiwa katika kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akizungumza wakati wa kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 (kushoto) ni Naibu Meya wa Manispaa hiyo Mhe Ramadhan Kwangaya na (kulia) ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo 
Mstahiki Meya Boniface Jacob (kushoto) katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayobo (kulia)
Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Yamo Wambura akitoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya matumizi ya fedha kwenye kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018


Na Mathias Canal, Dar es salaam

Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam kwa kauli moja limepitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kuungwa mkono na madiwani wote waliozuru katika mkutano maalumu wa baraza hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Kaimu Afisa habari na Uhusiano wa Manispaa hiyo Bi Maria Makombe imeeleza kuwa Katika mpango huo Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo inakadiria kukusanya/kupokea kiasi cha Tshs 128,611,616,805.100 ambazo zimeelekezwa katika matumizi ya mishahara, utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na matumizi mengineyo.

Fedha hizo zitatokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri, Ruzuku kutoka serikali kuu, Michango ya wananchi na wahisani wa Maendeleo.Aidha Halmashauri inatarajia kupokea kiasi cha Tshs 4,233,546,143.00 kutoka TAMISEMI kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara (Road Fund).

Katika fedha hizo chanzo cha makusanyo ya ndani ni Tshs 24,006,600,000.00 ambayo ni Sawa na asilimia 26% ya bajeti, Michango ya wananchi ni Tshs 500,000,000 Sawa na asilimia 1% ya bajeti, Mfuko wa barabara ni Tshs 4,233,546,143.00 Sawa na asilimia 4% ya bajeti na ruzuku kutoka serikalini na wahisani wa maendeleo ni Tshs 59,892,884,406.00 Sawa na asilimia 69% ya bajeti.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akisoma makisio ya bajeti ya Halmashauri ya Manispaa hiyo ameyataja maeneo yaliopata kipaumbele katika mpango huo kuwa ni pamoja na Kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Manispaa, pamoja na Ujenzi wa ofisi za Makao makuu ya Halmashauri ya Manispaa hiyo.

Vipaumbele vingine ni kuboresha miundombinu ya afya,shule za msingi na sekondari, kuboresha miundombinu ya maji, mifereji, taa za barabarani na kilimo mjini, Kuboresha hifadhi ya mazingira na ukusanyaji wa taka, Kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika upangaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo sambamba na Kuboresha mazingira ya wafanyabiashara ndogondogo.

Mhe Jacob ameeleza kuwa Manispaa hiyo ya Ubungo imejipanga kusimamia vyema uimarishaji wa mahusiano mazuri kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine, Kuendelea kujenga uwezo na ujuzi kwa watumishi katika utoaji wa huduma zilizo bora na zaharaka, kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na uwazi sambamba na Kujenga uwezo kwa viongozi wakiwemo waheshimiwa madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa katika kusimamia shughuli za wananchi.

Katika makisio ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo kwa 2017/2018 asilimia 72% itatumika kwa matumizi ya kawaida na asilimia 28% itatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Maombi maalumu yamewasilishwa kupitia bajeti hii ambapo ni pamoja na maombi ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa Makao makuu ya Halmashauri, Ujenzi wa Zahanati, Ununuzi wa magari, Malipo ya fidia kwa wananchi kwa maeneo yaliyochukuliwa na Halmashauri kwa ajili ya matumizi ya umma.

Mstahiki Meya alieleza Dira na dhima ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kuwa ni kuwa na jamii inayohamasika, inayokubalika ikiwa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake Mkurugenziwa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akizungumza wakati wa mkutano huoamesema kuwa Bajeti hiyo ina mambo mengi ambayo ni muhimu katika ustawi wa Manispaa hiyo hivyo ushirikiano wa pamoja kati ya madiwani na watumishi wa Manispaa hiyo itaimarisha mapato na uimara wa maendeleo katika jamii kwa kuwashirikisha wananchi.

MD Kayombo amebainisha kuwa Bajeti hiyo ina vipaumbele vingi lakini vile vilivyo muhimu zaidi vitafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo kwani ni sehemu ya kuimarisha nakukamilisha mipango ya mudamfupi katika Halmashauri.

Alisema kuwa makadirio ya mwaka 2017/2018 ya Tshs 128,611,616,805.00 yana ongezeko la kiasi cha Tshs 12,565681,576.01 ambapo Bajeti hii imepanda kwa asilimia 10 ukilinganisha na makisio ya Bajeti ya mwaka 2016/2017 ambayo yalikadiriwa kuwa ni Tshs 116,045,935,228.99.

Vipaumbele vya bajeti hii ya mwaka 2017/2018 ya Manispaa ya Ubungo vimewekwa katika sekta mbalimbali, ambapo Halmashauri imelenga kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, Kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kutoa huduma kwa kujenga ofisi za Halmashauri, Kuboresha utoaji huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa wakazi, Kutoka mikopo kwa wajasiriamali, Kuboresha usafi wa mazingira na Kuboresha miundo mbinu ya barabara, Shule na Afya.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania