CURRENT NEWS

Tuesday, March 21, 2017

IKUNGI YAZINDUA AWAMU YA PILI UANDIKISHAJI WA VITAMBULISHO VYA TAIFA.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akimkabidhi kitambulisho cha Taifa afisa Tarafa ya Sepuka Victor kavusha.
Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akimkabidhi kitambulisho cha Taifa kaimu Mkurugenzi wa halmashauri  hiyo Haika Massawe.


 Afisa wa NIDA wilaya ya Ikungi Agnes Mtei akitoa Taarifa ya zoezi la uandikishaji wa kitambulisho cha Taifa kwa Mkuu wa wilaya hiyo Miraji Mtaturu.
Mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Ikungi(OCD)Fortunatus Biaka akikabidhiwa kitambulisho cha Taifa na mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akimkabidhi kitambulisho cha Taifa katibu tawala wa wilaya hiyo Winfrida Funto.

Afisa Mamlaka wa Vitambulisho vya Taifa(NIDA) wilaya ya Ikungi Agnes Mtei akimkabidhi kitambulisho cha Taifa mkuu wa Wilaya hiyo Miraji Mtaturu.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akionyesha kitambulisho cha Taifa baada ya kukabidhiwa rasmi katika uzinduzi wa awamu ya pili ya uandikishaji wilayani humo.
                   .....................................................................................................................................................................................
MKUU wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu amezindua awamu ya pili ya uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa huku akiwataka viongozi na watendaji wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa maafisa uandikishaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA)ili zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi.

Uzinduzi wa awamu hiyo unafuatia baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza iliyoanza mwezi octoba mwaka jana na kufanikiwa kusajili watumishi wapatao 2,227.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mtaturu amesema zoezi hilo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi hivyo ni wajibu wa viongozi kuwahabarisha na kuwahamasisha wananchi kushiriki ili hatimaye lengo lililowekwa la kuwapatia wananchi wote  vitambulisho litimie.

“nimezindua awamu ya pili ya uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa,nawaomba viongozi wote na watendaji mtoe ushirikiano wa kutosha kwenye maeneo yenu,na mtambue kuwa wakati zoezi hili likiendelea ofisi zitakazotumika ni za vijiji hivyo hamasisheni watu wajitokeze,”alisema Mtaturu.

Kwa upande wake afisa uandikishaji kutoka NIDA Agness Mtei alisema awamu hii ya pili itakuwa na hatua nne lengo likiwa ni kuandisha wananchi wapatao 188,832 ambapo awamu ya kwanza wanatarajia kusajili wananchi 45,599 kutoka kata sita katika tarafa ya Ikungi.

“Awamu ya pili tunatarajia kusajili wananchi 54,887 katika kata nane Tarafa ya ihanja,awamu ya tatu wananchi 49,035 kutoka kata saba tarafa ya Sepuka na awamu ya nne wananchi 35,311 kutoka kata saba tarafa ya Mungaa,”alisema Mtei.

Alimshukuru mkuu wa wilaya kwa ushirikiano aliowapa toka wameanza zoezi hilo na kusema kwa kuanza wataanza kugawa fomu za usajili kwa wananchi wapatao 6,471 kutoka vijiji vya Ikungi,Ighuka na Mbwanjiki ambao wamefikisha umri wa miaka 18.

Makamu mwenyekiti wa halmashauri akizungumza kwa niaba ya madiwani na wadau aliwashukuru kwa kushiriki uzinduzi na kuahidi kutoa ushirikiano kwenye maeneo yao ili zoezi hilo lifanikiwe kama lilivyopangwa.

Jumla ya vitambulisho 2,075 viligawiwa katika uzinduzi huo huku kauli mbiu ikiwa Vitambulisho vya Taifa kwa Maendeleo ya Taifa.
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania