CURRENT NEWS

Sunday, March 12, 2017

JESHI LA POLISI PWANI LAWAKAMATA WATU 20 KWA KOSA LA UUZAJI DAWA ZA KULEVYA

KAMANDA  wa polisi mkoani Pwani, Boniventure Mushongi, akionyesha vifaa vilivyotumika katika matukio mbalimbali ya kiuhalifu mkoani hapo, ikiwemo shortgun, bastola, risasi, visu na vingine. (picha zote na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
JESHI la polisi Mkoani Pwani linawashikilia watu 20 kwa kosa la  kuhusika na uuzaji wa dawa  mbalimbali za kulevya ikiwemo heroin,mirungi na bangi .
Aidha limekamata nyara za serikali ,meno ya tembo sita thamani yake mil.98.100 na vipande 56 vya ngozi ya mbalawa .
Jeshi hilo pia limefanikiwa kukamata magunia ya bangi 28, puli 270 ,heroin kete 700 ,lita  522 za pombe ya moshi (gongo) na mitambo saba ya kutengeneza pombe hiyo,misokoto 52 ,kete 2,853 na mirungi milaa 94 .
Akizungumzia juu ya matukio hayo ,kamanda wa polisi mkoani Pwani, Boniventure Mushongi alisema, pia wamewakamata wahamiaji haramu 153 ambapo kati ya hao saba walikutwa wakisafirishwa kwenye gari namba T.568 CZG .
Alieleza ,kuna mazao ya misitu yasiyokuwa  na vibali nayo yamekamatwa ikiwa ni pamoja na mkaa magunia 71 na ambao 117 ,sukari viroba 23 vya kg hamsini na mchele viroba 12 vya kg 12 ,simu za mkononi 29 na nondo  tani  10.
Hata hivyo ,kamanda Mushongi, alisema mafanikio hayo yametokana na operesheni iliyofanyika  ndani ya wiki mbili baada ya kutokea tukio la  mauaji ya aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Liwale Ephraim Mfingi Mbaga (54).
"Katika operesheni hiyo wamekamatwa watu 15 ambao wamekiri kujihusisha na matukio ya uporaji na mauaji kwenye matukio mbalimbali mkoani hapo"
"Kadhalika wahalifu hao walikiri kujihusisha na matukio ya uvamizi na kusababisha vifo kwa Zawadi Dephara na Edward Chamuhene wote wawili wakiwa ni wakazi wa Misugusugu na Mtengi Mabuga mkazi wa Boko " alisema.
Kamanda Mushongi, alifafanua kuwa bastola mack IV moja yenye namba 1944 na risasi zake tatu ,bastola moja yenye namba A.1944 na risasi zake nne, short gun mbili nazo  zimekamatwa.
Alisema walifanikiwa kuipata  baada ya kutelekeza kwenye tukio la  ujambazi kufuatia aliyekuwa akiimiliki silaha hiyo kujeruhiwa wakati wa tukio hilo huko maeneo ya Misufini ,Mlandizi .
"Ikiwa imekatwa mtutu model 305 KB 12 na shortgun ya pili yenye namba 30102 pamoja na silaha aina ya gobole moja na risasi zake 19.
Kamanda Mushongi ,alibainisha ,tangu jan 2017  hadi sasa wamefanya operesheni katika maeneo mbalimbali ya mkoa na kukamata watuhumiwa 579 walifanya makosa mbalimbali .
Alisema wanaendelea na operesheni hiyo ambayo imeanza na wamejipanga kukabiliana na uhalifu wa aina yoyote.
Mwisho
 
Copyright © 2014 Mkono Wangu Production Designed by EvMak Tanzania